Breaking News

Your Ad Spot

Jun 12, 2015

TFF YA MALINZI YATOA OFA KUBWA' KWA WAZAZI WA SIMON MSUVA

Rais wa TFF Jamal Malinzi akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa tuzo jana usiku
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kwa Rais wake Jamal Malinzi, jana usiku lilitoa ofa kwa wazazi (baba na mama) wa Simon Msuva kuhudhuria mechi mbili za timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ itakapokuwa ikicheza dhidi ya Uganda kwenye michezo ya awali kuwania kufuzu kushiriki michuano ya Afrika inayoshirikisha wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).
Malinzi ametoa ofa hiyo kwa wazazi wa Msuva ambaye jana alitangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu ya soka Tanzania bara iliyomalizika Mei 9 mwaka huu ikiwa kama zawadi na shukrani kwa wazazi hao mara baada ya wazazi wa Msuva kueleza njia ndefu aliyopita mtoto wao kufikia mafanikio anayoyapata hivisasa na wao kusimama nyuma yake kwa kila jambo gumu na rahisi alilopitia kijana wao.
Baba yake Simon Msuva (mzee Msuva) akiwa ameinua juu tuzo ya mfungaji bora wa ligi iliyokwenda kwa Simon Msuva, (kulia kwake) ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Juma Nkamia na (kushoto kwake) ni mama yake Simon Msuva
Baba yake Simon Msuva (mzee Msuva) akiwa ameinua juu tuzo ya mfungaji bora wa ligi iliyokwenda kwa Simon Msuva, (kulia kwake) ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Juma Nkamia na (kushoto kwake) ni mama yake Simon Msuva


Malinzi amesema kuwa, amevutiwa na jinsi wazazi hao walivyosimamia na kukilea kipaji cha mtoto wao hivyo, TTF imeamua kuwapongeza kwa hatua hiyo na itagharamia kila kitu ili wazazi wa Msuva wapate kumuona kijana wao akicheza uwanjani kuiwakilisha Tanzania kwenye mechi dhidi ya Uganda itakayochezwa Zanzibar Juni 20 na ile ya marudiano itakayopigwa jijini Kampala huku TFF ikigharamia kila kitu kuanzia usafiri, gharama za viingilio, chakula na malazi ya wawili hao.
“Nimeguswa sana na maneno ya baba yake Msuva, ameongea maneno mazito sana ambayo yanaonesha ni jinsi gani amehangaika kutafuta mafanikio ya leo ambayo kijana wao (Simon Msuva) anayapata. Ni safari ndefu sana wamepitia na wanahitaji pongezi za dhati na ni mfano wa kuigwa na wazazi wengine”, alisema Malinzi huku akionekana kuvutiwa na wazazi wa Msuva.
“Kwasababu hiyo, kama TFF tunawaomba mhudhurie kumshuhudia mtoto wenu atakapokuwa akicheza kwenye timu ya Taifa wakati ikicheza dhidi ya Uganda mchezo utakaofanyika Zanzibar Juni 20, pia vilevile kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa jijini Kampala. TFF itagharamia kila kitu kuanzia usafiri, viingilio, malazi na chakula , karibuni sana kwenye mechi hizo”, alisema Malinzi.
Awali baba yake Msuva alisema, amepata changamoto nyingi sana wakati anahangaika huku na kule kuhakikisha mwanae anafanikiwa katika mchezo wa soka ambao alionesha kuuhusudu tangu akiwa kijana mdogo. Mzee Msuva alisema, ilifika wakati aligombana na mama yake Msuva kwasababu ya kumtafutia Msuva timu ya kucheza wakati mama yake alikua anahitaji Msuva aelekeze nguvu zake zote kwenye elimu akiamini ndiyo itamletea mafanikio maishani.
“Nimehangaika sana na Msuva kabla hajapata mafanikio aliyonayo leo, ilifikia wakati nagombana na mama yake kwasababu ya mpira. Mama yake Msuva alikuwa akitaka mtoto aelekeze nguvu zote shule lakini mimi nilikuwa nyuma ya Msuva kuendeleza kipaji chake cha kucheza mpira alichokionesha tangu akiwa mdogo. Sikumzuia kwenda shule, ila nilikuwa nahakikisha anapata pia nafasi ya kucheza mpira”, alisema mzee Msuva.
Wazazi wa Simon Msuva wakiwa wameshika tuzo ya mtoto wao mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Mh. Juma Nkamia aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo
Wazazi wa Simon Msuva wakiwa wameshika tuzo ya mtoto wao mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Mh. Juma Nkamia aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo
“Nimezunguka naye kwenye timu nyingi sana nikimpeleka akapate nafasi ya kucheza kabla hajatua Yanga ambapo wengi wametambua uwezo wake akiwa hapo. Kwakweli namshukuru sana Mungu kwa mafanikio haya aliyopata kijana wetu lakini naishukuru pia Yanga na watu wengine wote waliochangia mafanikio haya ya Msuva”, aliongeza mzee Msuva.
Msuva yupo na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo imepiga kambi nchini Ethiopia kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri utakaopigwa nchini Misri Jumapili Juni 14 mwaka huu kuwania kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON). Jana aliwakilishwa na wazazi wake kwenye hafla ya ugawaji tuzo kwa wachezaji, timu, makocha na waamuzi waliofanya vizuri kwenye ligi ya msimu wa 2014-2015 iliyomalizika hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages