Breaking News

Your Ad Spot

Jun 8, 2015

WIZARA YA NISHATI NA MADINI YAZINDUA HUDUMA ZA LESENI KWA NJIA YA MTANDAO - MAOMBI NA MALIPO YA LESENI KUFANYIKA KWA MTANDAO


????????????????????????????????????
Kikundi cha Ngoma za Asili cha Simba kutoka Dodoma (kushoto)  kikitumbuiza mbele ya  Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene (kulia katikati, aliyevaa koti la kahawia) kabla ya uzinduzi wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao uliofanyika mjini Dodoma.
????????????????????????????????????
Kamishna Msaidizi wa Madini- Kitengo cha Leseni, Mhandisi John Nayopa (Kulia)  akielezea mfumo wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao  unavyofanya kazi kabla ya kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene (wa pili kutoka kushoto, aliyekaa meza kuu).
????????????????????????????????????
Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi Paul Masanja (Kulia) akielezea mafanikio  katika uboreshaji wa huduma za utoaji leseni kwenye uzinduzi huo.
????????????????????????????????????
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akisoma hotuba ya uzinduzi wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao.
????????????????????????????????????
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (katikati) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa huduma za leseni kwa njia  ya mtandao. Wa pili kutoka kulia ni Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi Paul Masanja na wa kwanza kushoto  mbele ni Kamishna Msaidizi wa Madini- Kitengo cha Leseni, Mhandisi John Nayopa.
????????????????????????????????????
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (wa nne kutoka kulia, waliokaa mbele); Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi Paul Masanja ( wa tano kutoka kulia, waliokaa mbele) na Kamishna Msaidizi wa Madini- Kitengo cha Leseni, Mhandisi John Nayopa ( wa pili kutoka kushoto, waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini waliohudhuria uzinduzi huo.
…………………………………………………………………
Greyson Mwase na Samuel Mtuwa, Dodoma
Wizara ya Nishati na Madini imezindua mtandao utakaowezesha wachimbaji wa madini kutuma maombi ikiwa ni pamoja na kufanya malipo ya leseni za madini unaojulikana kwa jina la Online Mining Cadastre Transactional Portal (OMCTP).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mtandao huo iliyofanyika mjini Dodoma, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema kuwa lengo la mtandao huo ni kuwezesha shughuli za uchimbaji madini kufanyika katika uwazi na kukomesha rushwa.
Akielezea hatua mbalimbali katika uboreshaji wa huduma za leseni zilizopitiwa na Wizara Simbachawene alisema mwaka 1990 leseni zilishughulikiwa kwa njia ya mkono hadi kufikia mwaka 2005 ambapo Wizara ilianzisha mfumo wa kompyuta katika utoaji wa leseni uliojulikana kwa jina la MapInfo ambao bado ulitegemea uchambuzi kwa njia ya mkono.
Alisema ili kuboresha huduma ya utoaji wa leseni za madini, mwaka 2007 Wizara ilianzisha mfumo wa utoaji wa leseni za madini uliojulikana kama Mining Cadastral Information Management System (MCIMS) ambao uliwezesha ofisi za madini kuunganishwa kwa njia ya mtandao na kuwezesha uchambuzi wa maombi ya leseni kufanyika kwa njia ya kompyuta.
Alisema mfumo huo ulirahisisha sana upokeaji na uchambuzi wa maombi ya leseni na kurahisisha usimamizi wa leseni za madini.
Aliendelea kusema kuwa kupitia mfumo huo Wizara imeweza kupokea na kuchambua wastani wa maombi 1,400 ya leseni kubwa na 5,000 ya uchimbaji mdogo kwa mwaka.
Alisema mfumo huo umewezesha utolewaji wa wastani wa leseni 500 kubwa za madini na leseni zipatazo 1,500 za uchimbaji mdogo kila mwaka.
Waziri Simbachawene aliendelea kusema kuwa kuanzia mwaka 2010 Wizara iliendelea kuboresha mfumo wa flexicadastre chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali ya Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Alisisitiza kuwa maboresho hayo yalikuwa ni pamoja na kuwezesha uondoaji wa mlundikano wa maombi ya leseni, kuhuisha takwimu za leseni za madini na pia kuweka tovuti maalumu iliyowezesha wananchi kupata taarifa ya leseni za madini, maboresho yaliyochochea ari ya wananchi kufuatilia masuala ya leseni kwa njia ya mtandao, na kuweka uwazi katika usimamizi wa sekta ya madini kwa mujibu wa Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Nchini (TEITI)
Aliongeza kuwa kufikia Mei, 2015 jumla ya leseni 3,500 za utafutaji mkubwa wa madini, leseni 14 za uchimbaji mkubwa wa madini, leseni 389 za uchimbaji wa kati na leseni 39, 921 za uchimbaji mdogo wa madini zilitolewa.
Alisisitiza kuwa kwa sasa Wizara imeamua kuboresha huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao kama utekelezaji wa agizo la serikali la kuhakikisha kuwa malipo ya serikali yanafanyika kwa njia ya kielektroniki.
Simbachawene aliongeza kuwa mfumo huo mpya utawawezesha wateja waliosajiliwa kutuma maombi, kuhakiki taarifa za leseni wanazomiliki, kutuma taarifa za utendaji kazi na kufanya malipo ya leseni na mrabaha kwa njia ya kielektroniki.
Alisema mfumo huu pia utawawezesha wateja kuoanisha ramani za maeneo ya leseni na ramani za kijiolojia zilizoandaliwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
Aidha, Waziri Simbachawene aliwataka wamiliki wa leseni na wananchi wote kwa ujumla kujisajili katika mfumo huo kwa kuwa lengo la Wizara ni kuhakikisha kuwa huduma zote za leseni zinakuwa kwa njia ya kielektroniki ifikapo Agosti 31, mwaka huu.
Pia aliwataka makamishna wa madini pamoja na watendaji wake kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu mzuri wa kuwasajili wachimbaji wadogo ili nao waweze kutumia huduma hizo la kielektroniki bila kikwazo.
Wakati huo huo akielezea faida za mfumo huo, Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi Paul Masanja alisema kuwa mfumo huu unawawezesha wateja waliosajiliwa kutuma maombi, kuhakiki taarifa za leseni wanazomiliki, kutuma taarifa za utendaji kazi, kupata historia ya leseni zao, kuhuisha leseni zao, kuongeza ukubwa wa maeneo ya leseni zao na kufanya malipo ya leseni na mrabaha kwa njia ya kielektroniki.
Mhandisi Masanja aliongeza kuwa mfumo huu utawawezesha wamiliki wa leseni kuwa na usimamizi wa leseni zao kwani utakuwa ukimjulisha mmiliki wa leseni lini leseni yake inatakiwa kulipiwa na lini leseni yake itaisha
“Mfumo huu pia umesheheni takwimu mbalimbali za madini ikiwa ni pamoja na ramani za maeneo ya leseni na ramani za kijiolojia zilizoandaliwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)” Alisema Mhandisi Masanja
Aliongeza kuwa, mfumo huu utawapunguzia mzigo watalam wa Wizara kwa kuwa wateja wenyewe wataingiza maombi ya leseni na hivyo wataalam kufanya uchambuzi kwa haraka zaidi na kupata muda wa kutosha kusimamia leseni zilizopo.
Alisisitiza kuwa mfumo huu umelenga kuondoa upotevu wa fedha za serikali kutokana na vitendo vya rushwa na makosa mengine ya kibinadamu.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya usajili wa wateja katika mfumo huo, Mhandisi Masanja alisema tangu kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 2013 hadi sasa ni wateja 140 tu kati ya wateja wapatao 400 wamesajiliwa na wachimbaji wadogo 20 kati ya wamiliki wapatao 4,000 wamesajiliwa katika mfumo huo na kuwataka wadau wote waone umuhimu wa kujisajili na kutumia huduma hizi ili kuondoa matatizo ya ucheleweshaji wa kushughulikia maombi yao.
Mhandisi Masanja aliongeza kuwa kuanza kutumika kwa mfumo huu kunaiweka nchi ya Tanzania katika nchi chache za Afrika zilizo na mfumo wa kisasa wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages