.

TANZANIA YAPATA MSAADA WA MAGARI MAALUMU 50 ILI KUONGEZA NGUVU KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UJANGILI

Jul 20, 2015

NYA1
Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe. Lazaro Nyalandu akiwa na  Balozi wa China nchini,   Lu  Youqing   wakizindua magari maalumu 50 yatakayotumika katika vita dhidi ya Ujangili.
NYA2
Haya ni baadhi ya magari maalumu yaliyotolewa na  Serikali ya China  yatakayotumika katika vita dhidi ya Ujangili.  Mwingine ni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhem Meru.
…………………………………………………………………………….
Serikali  ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekabidhiwa msaada wa magari maalumu  50 pamoja  na  vifaa vya vingine 417  na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ili kuongeza nguvu  katika mapambano dhidi ya Ujangili.
Katika makabidhiano hayo , Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa  magari 50 yenye thamani ya  bilioni 2.6  yakiwemo magari yenye matairi matatu yenye uwezo ya kutembea sehemu yoyote ya pori hata mahali pasipo na barabara  ili kuweza kuwasaidia Askari wanyamapori  kukabiliana na majangili watakaothubutu kutoroka.
Mbali ya magari hayo , China  imetoa  vifaa maalumu  vya kukagua  makontena ili  kubaini endapo yamebeba nyara za Serikali ambapo kwa awamu hii ya kwanza vifaa hivyo vitaanza kutumika katika Bandari ya Dares Salaam.
Akizungumza  jana jijin Dares Salaam muda mfupi  mara baada ya  makabidhiano hayo , Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe. Lazaro Nyalandu alisema magari hayo maalumu yatasaidia Askari wanyamapori kumudu kazi  kwa kushirikiana na vyombo vya usalama  katika  kuwakamata majangili popote walipo.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya watu wa China imeonesha njia kwa Mataifa  makubwa kwa kuisaidia Tanzania kupambana na  Ujangili,  ‘’ Serikali ya Tanzania haina mzaha na mtu yeyote anayejihusisha na Ujangili, ‘’ Mhe, Nyalandu alisema.
‘’Magari haya tuliyokabidhiwa leo yatapelekwa moja kwa moja kwenye  maeneo ya kazi  na kamwe  hayatabaki hapa kwa ajili ya matumizi ya maofisa,, Huu ni mpango endelevu  wa  vitendea kazi  kwa ajili ya Askari wanyamapori ili kuwasaidia kumudu kazi ya kupambana na majangili’’ Mhe. Nyalandu alisema.
‘’Serikali inatoa onyo kwa wananchi wanaowahifadhi majangili na wanaoshirikiana na majangili ninawasihi waache mara moja’’  Mhe. Nyalandu alisisitiza
Mhe. Nyalandu amesema  vita dhidi ya Ujangili ni vita  ya kidunia hivyo Tanzania imekuwa  ikishirikiana  na Askari wa  Kimataifa ( Interpol)  pamoja  na kupata  msaada  kutoka kwa mataifa makubwa katika kutokomeza mtandao wa Ujangili.
Akizungumza katika  makabidhiano  hayo.  Balozi wa China nchini  Tanzania Bw. Lu  Youqing  amesema  nchi yake itaendelea kuisadia Tanzania katika vita dhidi ya Ujangili kutoka na tatizo kubwa la ujangili  lililopo licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania.
‘’Tumeamua kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Ujangili kutokana na si Tanzania tu inayoathirika na tatizo la Ujangili bali ni tatizo linaloathiri hata mataiafa makubwa Makubwa ikwemo sisi’’ Balozi wa China nchini Tanzania,  Bw. Lu  Youqing  alisema.
Alisema wameanza kuonyesha kwa vitendo kushirikiana na Tanzania katika vita dhidi ya Ujangili kwa kutoa  vifaa vya kisasa ambavyo vitawawezesha Askari  wanyamapori kuweza kuwasiliana kwa urahisi  katika maeneo yao ya kazi.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª