Breaking News

Your Ad Spot

Sep 18, 2015

TANZANIA NA NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akihutubia katika ufunguzi rasmi wa Semina ya Ushirikiano wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency ya Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanna-Marie Kaarstad na wadau wengine katika sekta ya biashara na uwekezaji kutoka Norway na hapa nchini.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Maeland (kulia) akimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo. Kushoto ni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula na katikati ni  Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Kaarstad. 
Waziri Membe akiendelea kuzungumza
Waziri wa Biasha na Viwanda nchini Norway Mhe. Monica Maeland naye alipata fursa ya kuzungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Maeland yupo nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania nchini Norway. Pia wakati wa ziara hiyo Mhe. Maeland amezindua mtambo wa mbolea wa Yara ulioko kwenye Bandari ya Dar es Salaam na pia atatembelea Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga (kulia) na mmoja wa wadau katika semina hiyo Bw. John Ulanga (kushoto) wakifuatilia Hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa na Mhe. Membe na Mhe. Maeland (hawapo pichani). 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Tunsume Mwangolombe (katikati) naye akifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo.
Sehemu ya wadau wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo 
Semina ikiendelea
Waziri Membe (katikati) na Waziri Maeland kwa pamoja na wajumbe waliofuatana nao wakiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kumaliza ufunguzi wa semina.

DSC_0246 Waziri Membe (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya  faida ya semina hiyo ya wafanyabiashara wa Tanzania na Norway.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.(Picha na Reginald Philip).
 Na Mwandishi wetu
Waziri wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameisifu Serikali ya Norway kwa kuwa mshirika wa karibu wa maendeleo wa Tanzania hususan katika sekta za biashara na uwekezaji.
Waziri Membe alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Abdallah Kigoda wakati akifungua rasmi semina kuhusu kuimarisha ushirikiano wa Kibiashara  na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam leo.
Katika ufunguzi huo ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi, Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa kidiplomasia kwa miaka mingi lakini sasa nchi hizi zimeamua kushirikiana zaidi katika masuala ya uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi zote mbili.
Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imefaidika na  ushirikiano na Norway katika sekta mbalimbali ambapo nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuisaidia Tanzania kupambana na umaskini na kukuza uchumi. Hata hivyo alisema umefika wakati sasa nchi hizi mbili zinufaike kupitia biashara na uwekezaji ambapo nchi zote zina fursa nyingi katika maeneo hayo ikiwemo gesi na mafuta, kilimo na madini.
Mhe. Membe alisema kuwa kufanyika kwa semina hii itakayowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji itaongeza thamani katika uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili ambapo Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Norway ambayo ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha zaidi gesi asilia na mafuta duniani. Hivyo aliwaasa Watanznaia kutumia semina hiyo kujifunza ili kuimarisha sekta ya nishati ya hapa nchini.
“Semina hii ni fursa kwa Kampuni za Tanzania na Norway kujifunza na kubadilisha uzoefu na mawazo ya namna bora ya kuboresha sekta za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili” alisema Waziri Membe.
Akizungumzia biashara inayofanyika kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania inatakiwa kuongeza biashara yake nje ya nchi ili kuimarisha uchumi wake. Alieleza kuwa kwa sasa biashara kati ya Tanzania na Norway imeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 6.9 mwaka 2014 kwa bidhaa zilizozwa Norway kutokea Tanzania ikiwemo kahawa, chai, viungo, maua, mbogamboga, mbao na madini.
Kwa upande wa bidhaa kutoka Norway, Tanzania imenunua kwa ongezeko la kutoka bilioni 22.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 73 mwaka 2014. Bidhaa hizo ni pamoja na dawa za binadamu na bidhaa za viwandani.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Monica aliipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo na ukuaji wa uchumi ambao umefikia asilimia 7. Alieleza kuwa Tanzania itafikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa vile inayo dhamira ya dhati na imejipanga kupitia uvumbuzi wa gesi na mafuta, nguvukazi ya vijana na mageuzi yaliyopo katika sekta ya uchumi.
Alieleza kuwa Norway ipo tayari kuendelea kuisadia Tanzania katika sekta ya gesi na mafuta kwa vile nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo hususan katika masuala ya teknolojia. Aidha, aliongeza kuwa Tanzania ni mshirika wa kweli wa Norway katika maendeleo hivyo nchi yake itashirikiana kikamilifu na Tanzania.
“Kuna msemo maarufu unasema kama unataka kwenda mbio nenda peke yako, lakini kama utanaka kufika mbali nenda pamoja na mwenzako. Hivyo Norway inataka kwenda pamoja na Tanzania ili kuziwezesha nchi hizi kufika mbali kimaendeleo” alisisitiza Mhe. Monica.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa nchi hizi mbili kukuza biashara kwa kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu kwani ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu.
Semina hiyo ambayo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Norway, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ilihudhuriwa na Makampuni 34 kutoka Norway na Tanzania na pia wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages