Breaking News

Your Ad Spot

Oct 2, 2015

MAREKANI YAONYA KUHUSU MASHAMBULIYO YA URUSI

Wanachama wa muungano unaoongozwa na Marekani kukabiliana na wapiganaji wa Islamic State wameitaka Urusi kusitisha mashambulio kutoka angani wakisema yanadhuru makundi yanayompinga Bashar al-Assad pamoja na raia.
Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa Ijumaa, Marekani, Uingereza, Uturuki na mataifa mengine ya muungano huo yalisema mashambulio ya Urusi yatazidisha kuwepo kwa makundi yenye itikadi kali
Urusi, ambayo kwa mujibu wa mashahidi ilianzisha tena mashambulio Ijumaa, inasema inalenga IS.
Afisa mkuu wa Urusi anasema mashambulio hayo huenda yakaendelea kwa miezi mitatu hadi mine.
Alexei Pushkov, mkuu wa kamati ya mashauri ya kigeni katika bunge la Urusi, aliongeza kuwa Marekani ilikuwa tu “ikijifanya” kuangushia mabomu IS na akaahidi kwamba kampeni ya Urusi itafanikiwa zaidi.
Jeshi la angani la Urusi lilianza kushambulia maeneo ya Syria Jumatano.
Jeshi la Syria linasema Urusi ilitekeleza mashambulio 18 tangu Alhamisi jioni. Inasema baadhi ya mashambulio hayo yalitekelezwa Hama na Idlib, mikoa ambayo haina wapiganaji wa Islamic State kwa wingi.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema ndege zake za kijeshi zilishambulia ngome ya IS eneo la Raqqa Alhamisi. Wanaharakati wanasema wapiganaji kadha wa IS waliuawa huko.
Mashambulio hayo ya ndege Syria ndiyo operesheni ya kwanza ya kijeshi wa Urusi nje ya eneo la uliokuwa Muungano wa Usovieti tangu kumalizika kwa Vita Baridi.
Onyo la mataifa ya muungano huo unaoongozwa na Marekani limetolewa huku viongozi wa Ufaransa na Urusi wakitarajiwa kukutana baadaye Paris.
Mkutano huo uliitishwa kujadili juhudi za kutafuta amani Ukraine, lakini sasa hilo huenda likagubikwa kwa Syria.
Upinzani nchini Syria umedai makundi ya waasi yanaompinga Rais wa Syria Bashar al-Assad, ambaye ni mshirika wa Urusi, nadiyo yanayoumizwa Zaidi na mashambulio ya Urusi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, akiongea katika makao makuu ya UN New York, alisema Urusi itashambulia pia makundi mengine ya kigaidi likiwemo al-Nusra Front, lenye ushirika na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
"Hatuungi mkono kundi lolote. Tunapigana na ugaidi,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages