.

NENO LA LEO : MZEE MWINYI NA CCM 'B'

Oct 24, 2015

Ndugu zangu,
Afrika mvua hainyeshi ghafla. Mzee Ali Hassan Mwinyi ni mmoja wa viongozi wa nchi hii ninaowaheshimu sana. Naamini pia, Rais Mstaafu Mwinyi anayeheshimika na wengi.
Nilikuwepo viwanja vya Jangwani siku CCM ilipofanya uzinduzi wa kampeni zake. Nilimwona na kumsikia kwa masikio yangu Mzee Mwinyi akisema , kuwa kuna CCM ' A' na CCM ' B'. Na kwama kama CCM ' A' ipo kwanini mchague CCM ' B'.
Kwa kuangalia kampeni za UKAWA, ndipo maneno ya Mzee Mwinyi yalipodhihiri. Kampeni za mgombea Urais wa Ukawa zinazohitimishwa leo sambamba na za CCM, kimsingi zilitawaliwa na Wana- CCM wa zamani.
Ni viongozi wa zamani wa CCM aina ya Edward Lowassa, Sumaye, Guninita, Mgeja, Masha, Kingunge na baadhi wengine. Kuna wakati ilikuwa mtu anahangaika kuitafuta safu ya upinzani ya wapiganaji aina ya John Mnyika, Godbless Lema, Tundu Lissu, Halima Mdee na wengine. Inatoa tafsiri pia kuwa, upinzani, hadi miezi mitatu iliyopita, ulikuwa haujajiandaa kuunda Serikali kwa kutegemea safu yake.
Ndugu zangu,
Duniani hapa dalili ya mvua ni mawingu. Afrika mvua hainyeshi ghafla. Mwenye kutamka kuwa mvua imenyesha ghafla, huyo hajajisumbua kuangalia juu mawinguni. Afrika hata kusanyiko la mawingu ya mvua lina dalili zake. Wazee wetu wa zamani walikuwa na maarifa ya kuona dalili za kusanyiko la mawingu ya mvua. Ninachotaka kusema hapa ni hiki; kila jambo ni wakati na dalili.
Na tunapokumbushana umuhimu wa kusoma ishara za nyakati hatuna maana ya kuziangalia saa zetu za mikononi au ukutani. Ni kuyaangalia matendo yetu ya sasa na hivyo basi umuhimu wa kuzisoma ishara za mambo yatakayotokea.
Pale viwanja vya Jangwani kwenye ufunguzi wa kampeni za CCM , Mzee Mwinyi alizungumzia juu ya uwepo wa CCM ' A' na CCM ' B'.
Yumkini moja ya changamoto ya Serikali ijayo ya John Magufuli ni namna ya kuishi maisha ya kisiasa na kufanya kazi huku kukiwa na upinzani unaotoka kwa wapinzani asilia, na wale wa kutoka CCM' B'.
Ni Neno La Leo.
Maggid,
Iringa

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช