Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora . Angella Kairuki (kushoto) akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi
za Wakala jijini Dar es salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora. Angella Kairuki (katikati) akiwasili Ofisi za Wakala ya Serikali
Mtandao kwa ziara ya kikazi jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Angella Kairuki (kushoto) kuhusu utendaji wa wakati
kwa ziara ya kikazi ya Angella
Kairuki katika Ofisi za Wakala leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Uratibu
wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao, Benjamin Dotto akitoa
ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki (kulia) mara alipotembelea kituo cha
ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini jijini Dar es salaam leo.
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Serikali imepiga marufuku matumizi ya
Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za
Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa
Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa
lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es
salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe.Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala
ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua
utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini.
“Sasa kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani
za Barua pepe za Serikali
,idadi hii ni ndogo lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa
taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na kuongeza kuwa
Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano
binafsi.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa
uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya
TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya
kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali.
Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa
Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha
kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma
zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa
Mawasiliano.
“Katika hili ninatoa siku 60 muhakikishe
kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili kwa wale watakaopuuzia hatua
zianze kuchukuliwa” Ameeleza Mhe. Angella.
Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa
Wakala hiyo kuweka mpango wa
kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga utaratibu wa
kuwarithisha uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji wa
Wakala hiyo.
Mhe. Kairuki amewataka kuwa wabunifu
katika kuanzisha mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha dhana ya Serikali
mtandao ili kupunguza
gharama hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala
mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.
Akizungumzia kuhusu ununuzi wa vifaa vya
TEHAMA serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya
ubadhirifu na matumizi mabaya ya
fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana
kwa bei ya kawaida.
“katika hili Serikali itachukua hatua kwa
yeyote atakayebainika katika upotevu wa mapato muhakikise mnazisaidia Wizara na
Taasisi mbalimbali za Serikali katika masuala ya ununuzi wa mifumo na vifaa vya
TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe na manufaa kwa wananchi na thamani halisi
ya fedha”
Amesema Serikali itaendelea kuboresha
utoaji wa huduma kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu
na kutoa wito kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa wabunifu katika kutengeneza
programu mbalimbali na mifumo salama itakayowasaidia wananchi kupata huduma.
Aidha, katika hatua nyingine ameitaka
e-Gov kuendelelea kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na majanga mbalimbali
yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala hiyo iendelee
kulifanyia kazi suala la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza kati ya
taasisi moja hadi nyingine ili huduma zote ziweze
kupatikana katika eneo moja na
kuondoa urudufu wa mifumo iliyopo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala
ya Serikali Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya utendaji wa
Wakala hiyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali toka
kuanzishwa kwake Julai 11, 2012 imeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa
Serikali Mtandao.
Amesema kuwa Wakala hiyo inaendelea
kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinawafikia wananchi kupitia mtandao mahali
walipo na kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la huduma zote za Serikali
kupatikana chini ya dirisha moja.
Aidha amesema kuwa Wakala ya Serikali
Mtandao itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya matumizi ya TEHAMA
katika Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali vinazingatiwa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269