Breaking News

Your Ad Spot

Dec 30, 2015

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PFOF. JUMANNE MAGHEMBE AKABIDHIWA RASMI OFISI LEO NA ALIYEKUWA WAZIRI WA WIZARA HIYO LAZARO NYALANDU

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akikabidhiwa taarifa ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo  Lazaro Nyalandu (wa pili kulia)  Dec 29, 2015 ofisini kwake Mpingo House. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Selestine Gesimba (kulia).
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) akizungumza na Waziri wa sasa wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru (kulia) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika Dec 29, 2015 katika ofisi za Wizara hiyo Mpingo House. Katika salamu zake Mhe. Nyalandu amepongeza uteuzi wa Prof. Maghembe ambapo amesema Mhe. Rais amefanya chaguo sahihi kwani Prof. Maghembe anao uwezo wa kufanya kazi nzuri katika Wizara hiyo.  
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akizingumza na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kulia) muda mfupi baada ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisini kwake,  Prof. Maghembe amempongeza  Nyalandu kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa Waziri wa Wizara ya Malisili na kuahidi kuanzia alipoishia katika kuhakikisha Maliasili za nchi zinatunzwa ipasavyo ikiwemo kupambana na changamoto zilizopo za ujangili na uharibifu wa misitu na maliasili kwa ujumla.
 
…………………………………………………………………..
 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri kabla yake Mhe.
Lazaro Nyalandu, Makabidhiano hayo yamefanyika  Makao Mkuu ya Wizara hiyo,
Mpingo House jijini Dar es Salaam.
 
Katika makabidhiano hayo Nyalandu
amekabidhi taarifa rasmi ya makabidhiano kwa  Waziri Prof. Jumanne Maghembe
kama ishara ya kukabidhi rasmi Ofisi ya Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
 
Makabidhiano hayo ambayo ni utaratibu
wa kiserikali wa kukabidhi ofisi umeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.
Adelhelm Meru, Naibu Katibu Mkuu, Selestine Gesimba,  baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo na
waandishi wa habari.
 
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo
  Nyalandu amempongeza Rais Magufuli kwa kumteua Prof.
Maghembe kuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili kwa kuwa ana sifa stahiki za
kuongoza Wizara hiyo nyeti.
 
Aliongeza kwa kusema kuwa Prof. Maghembe ana sifa
ya kuwa mhifadhi kwa kusomea na pia ni mhifadhi kwa asili yake hivyo Wizara
imepata mtu makini kwenye masuala ya Uhifadhi.

“Natambua umahiri wako katika masuala
ya uhifadhi nina imani utapambana na ujangili
pamoja na usafirishaji haramu wa magogo kwa kasi inayotarajiwa na
wananchi”. Alisema  Nyalandu.
 
Kwa upande wake, Waziri aliyechukua nafasi yake  Prof. Jumanne Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzuri na juhudi
aliozoonesha wakati  akiwa Waziri wa
Wizara hiyo katika kuhakikisha Maliasili zilizopo zinaendelea kuwepo kwa faida
ya kizazi cha sasa na kijacho.
 
Prof. Maghembe ameongeza kuwa kwa sasa vita kubwa iliyoko mbele yake ni vita dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa rasilimali za misitu kinyume cha sheria. Ameomba ushirikiano kwa wadau wote wa Maliasili nchini kumpa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anafanikiwa katika vita hiyo.
 
Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo ya
makabidhiano inaelezea kazi zilizokwisha kufanyika katika kipindi cha utawala
uliopita, kazi zinazoendelea na zilizopo kwenye mpango wa utekelezaji pamoja na
changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo
Ujangili na uvunaji pamoja na usafirishaji wa magogo. 
   
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages