Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (Pichani), amefurahishwa na hali ya chakula mkoani Ruvuma,
ikiwa kati ya mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi
nchini.
Akizungumza na viongozi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali jana jioni (Jumapili, Januari 3, 2016)
katika ukumbi uliopo Ikulu ndogo Songea, Waziri Mkuu ameutaka uongozi
wa mkoa kuhakikisha kuna upatikanaji wa masoko kwa mazao mbalimbali
pamoja na kuendelea kutoa msukumo kwa wananchi.
Pia, ameupongeza uongozi wa mkoa
huo kwa kutoa msukumo kwa wananchi na kufanyakazi, na kusema ni jambo
linalosaidia kupanda kwa pato la mtu mmoja mmoja, hata hivyo hakusita
kuwashukuru kwa mapokezi makubwa aliyopata.
“Nawapongeza sana wana Ruvuma kwa
kuongeza pato la ndani kutoka kutoka sh. 654,227, hadi kufikia
sh. 1,800,000 kwa kipindi cha mika 4 tuendelee kujiweka vizuri kwa
kuongeza pato la mtu mmoja mmoja” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa pia
amesisitiza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yote yenye mabonde ili
wakulima waweze kuvuna bila kutegemea sana kipindi cha masika. Amesema
ni lazima kuimarisha huduma muhimu na kusisitiza matumizi mazuri ya
fedha zinazopatikana katika mazao hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Said Thabit Mwambungu amesema zaidi ya asilimia 90 ya wananchi
wa Ruvuma hutegemea kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara
yakiwemo mahindi, mpunga ambao unalimwa sehemu za Tunduru na Songea
vijijini, korosho ambazo zinalimwa sehemu za Tunduru, Namtumbo, Nyasa,
Mbinga na Songea vijijinina tumbaku maeneo ya Namtumbo,Mbinga na Songea
vijijini.
Alisema, Ruvuma imekua ikizalisha
chakula kwa kiwango cha utoshelezi na ziada kwa kipindi cha mwaka 2012 –
2013, 2013 – 2014 hali hiyo imeendelea kuwa nzuri hadi kipindi cha
mwaka 2015 – 2016. Mahitaji yakiwa ni tani 469,172 na ziada ikiwa tani
1,950,111, ametaja baadhi ya sababu za ongezeko hilo la tani ni pamoja
na matumizi ya dhana bora za kilimo, matumizi ya pembejeo za kisasa na
urahisi wa upatikanaji wa pembejeo, aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye jana
(Jumapili, Januari 3, 2016) ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani
Ruvuma, kesho siku ya jumatatu atakuwa na shughuli za kufungua tawi
la Benki ya Posta mjini Songea, kukagua maghala ya Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya chakula (NFRA) kanda ya Songea na kukagua Makao Makuu ya
Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Kupitia ziara hii Serikali ina
lengo la kuona hali halisi ya utendaji wa shughuli za maendeleo kutoka
kwa watendaji mbalimbali, kuwatia moyo na kuweka msisitizo katika
maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika sekta ya Afya.

No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269