Breaking News

Your Ad Spot

Feb 5, 2016

CT-SCAN ILIYOPELEKWA MUHIMBILI ILIKUWA YA UDOM


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imekiri kwamba mashine ya CT Scan iliyofungwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilikuwa ni ya kituo cha kisasa cha kutolea huduma za afya cha Benjamin Mkapa kilichopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Akijibu swali la nyongeza bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Khamis Kigwangalla alisema mashine hiyo iliingia nchini kwa lengo la kupelekwa katika kituo hicho lakini ikapelekwa Muhimbili kutokana na kutokamilika kwa majengo ya kufungwa mashine hiyo katika kituo hicho.

Alisema, uamuzi huo waliuchukua pia kwa sababu hela ya kununua mashine nyingine ambayo itapelekwa kufungwa katika kituo hicho ilikuwepo na kwa sasa mchakato wa ununuzi unaendelea.

Dk Kigwangalla alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) aliyetaka jibu la Serikali kama ni kweli ilichukua mashine ya kituo hicho na kufunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ama ilinunua.

Awali katika swali la msingi msingi, Nkamia alitaka kujua mpango wa Serikali wa kununua mashine mpya ya CT -Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.

 Kuhusu hilo, Dk Kigwangalla alisema, Desemba mwaka jana Serikali ilipeleka mashine ya CT-Scan katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo inatumia teknolojia ya kisasa yenye X-ray tube mbili na uwezo wa kupiga picha ya 128 slice mara mbili.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages