Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Paul Makonda akizungumza leo na waandishi wa habari, Dar es salaam wakati alipozungumzia mpango wa
kuwasafirishwa walimu bure jijini humo (kulia) ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva, Shabani Mdemu na Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam, (Uwadar), William Masanja.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda wa pili (kushoto) akimsikiliza
Mwenyekiti wa Chama Chama Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es salaam, Said Mabrouk
wakati akizungumzia mwitikio wa wamiliki hao kuhusu
kuwasafirisha walimu ili kuunga mkono mpango wa Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kutoa
elimu bure hapa nchini.
……………………………………………………………………………………………………………….
Moja ya jambo ambalo serikali ya
awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa John Pombe Magufuri
imelifanya kuwa kipaumbele kikubwa kwenye mipango yake ya kimaendeleo ni
suala la uboreshaji wa sekta ya elimu nchini na ndio maana serikali
imeanza utekelezaji wa mpango huu kwa kufuta ada zote mashuleni.
Kimsingi ni ndoto hii ya
Mheshimiwa Raisi ambayo nina hakika kila mmoja wetu anaelewa ukubwa wa
faida zake kwenye ujenzi wa Tanzania mpya na yenye wasomi na wataalamu
wa kila namna tena wanaopatikana bila kuzingatia hali ya kipato cha
familia anayotokea mwanafunzi, iliyonifanya mimi kama msaidizi wake
katika nafasi ya ukuu wa wilaya nijiulize kila wakati juu ya ushiriki
wangu wa kuhakikisha inatimia kikamilifu. Maswali ambayo yamenifikisha
kwenye wazo la kuboresha sekta hii kwa kuchagua kufanya jambo ambalo
wakati serikali ikiendelea kupigania changamoto nyinginezo za kuboresha
ajira za walimu ikiwemo upandishwaji wa madaraja na mishahara, basi na
mimi katika nafasi yangu nishiriki kwenye mchakato huu mzima kwa kutoa
motisha ya usafiri wa bure kwa walimu wote wanaofundisha kwenye shule za
serikali zilizopo jijini Dar es Salaam.
Kwa ufupi ni kwamba, wazo hili
limejengwa juu ya msingi wa sababu kubwa tatu. Moja, kwa kuzingatia
changamoto za nauli za mara kwa mara wanazolazimika kuzilipa walimu ili
kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia kazi na pili, ni kuhakikisha
mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni tunakuwa sehemu ya juhudi
za Mheshimiwa Raisi za kuboresha maslahi na mazingira ya walimu ya
kufanyia kazi ili matarajio ya ndoto yake anayoipigania usiku na mchana
ya kutaka kuiona sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia. Na
tatu, ni kuwafanya walimu wa wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa
ujumla kama watumishi wenzangu wa serikali nao wanafaidi sehemu ya
matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati imedhamiria kubadilisha maisha
yao ili na wao waweze kubadilisha maisha ya vijana wetu kupitia taaluma.
Kwasababu hizo nilizozianisha
hapo juu ninaomba kuwatangazia walimu wangu wa shule zote za serikali
kuanzia za msingi mpaka sekondari ya kwamba, sasa watasafiri bure
wanapokwenda kutufundishia wadogo zetu na watoto wao. Hii ni baada ya
kufanya vikao na mazungumzo ya kina na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa
umma kupitia vyama vyao vya Darcoboa na Uwadar na hatimaye mazungumzo
hayo kuitimishwa na mkutano wa vyama vyote hivyo viwili vya wamiliki wa
vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali kuniunga mkono kwenye
utekelezaji wa wazo langu hili.
Kipekee na kwa unyenyekevu
mkubwa, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wamiliki hawa wa
vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi wa vyama vya Darcoboa na
Uwadar kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa ukizingatia kuwa
wao ni wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika sekta yao
ya usafirishaji, wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili wapate
uwezo wa kufanya biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao
wameseme ndio na wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo.
Utaratibu kwa walimu juu ya
utumiaji wa fursa ambayo tumeipata utakuwa kama ifuatavyo:- Moja,
nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi, kutoa
maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu
na wilaya nyinginezo za jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho
vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili, jina
la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na
saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu.
Nimewataka zoezi hili walifanye
na kulikamilisha ndani ya wiki moja ambapo baada tu ya kukamilika
itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu wote wa shule za serikali
jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda daladala bure ila tu kwa
siku za jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda wa saa kumi na moja asubuhi
mpaka saa mbili asubuhi na kati ya saa tisa mpaka saa kumi na mbili
jioni. Ingawa, kila mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake
alichotengenezewa kwenye shule yake pamoja na kile cha ajira ya
serikali.
Imetolewa na:-
Paul Makonda
Mkuu wa wilaya – Kinondoni.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269