Breaking News

Your Ad Spot

Feb 2, 2016

SERIKALI YA UGANDA YAWAKOSOA WAANGALIZI WA UMOJA WA ULAYA

Serikali ya Uganda inawashutumu baadhi ya maafisa wa Umoja wa Ulaya kwa kile inachosema wanaingilia mambo ya ndani, huku ikimtia nguvuni Jenerali David Sejusa kwa tuhuma za kujihusisha na siasa akiwa mwanajeshi.
Kundi la wangalizi 30 wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya lilianza shughuli wiki tatu zilizopita likifuatilia jinsi kampeni zinavyoendeshwa, kushauriana na wadau wa uchaguzi huo wakiwemo wagombea wa upinzani na pia vyombo vya usalama na Tume ya Uchaguzi, lakini msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo, amewaambia wanahabari kwamba serikali imegundua njama za baadhi ya waangalizi hao kushirikiana na maafisa wa Umoja wa Ulaya kupendelea upinzani.
Opondo alisema waangalizi hao wanafadhili "uanzishaji wa kituo kisicho rasmi cha kukusanyia na kuchuja matokeo ya uchaguzi."
Madai haya ya serikali yanayoibuka siku 17 tu kabla ya uchaguzi kufanyika, yanapelekea kuwepo kwa mazingira ya ukosefu wa imani miongoni mwa wadau mbalimbali kama suala zima la uchaguzi pamoja na matokeo ya zoezi hilo kuwa ya haki na huru.
Jenerali Sejusa akamatwa
Wakati huo huo, kitendo cha kumkamata aliyekuwa wakati mmoja mkuu wa vyombo vya ujasusi vya Uganda, Jenerali David Sejusa, kiliwashangaza wengi. Jenerali Sejusa, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Kaguta Museveni, alikamatwa hapo jana na kuzuiliwa katika kambi ya kijeshi ya Makindye nje kidogo ya jiji la Kampala.
Wakili wa jenerali huyo, David Mugisha, alisema mteja wake "hakuruhusiwa kushauriana na yeyote mkiwemo mawakili wake."
Huku mawakili hao wakielezea kutofahamu hasa sababu za kukamatwa kwa jenerali huyo ambaye amekuwa akiandamana na Dk. Kizza Besigye katika kampeni zake, msemaji wa serikali, Opondo, amefahamisha kwamba ni kuhusiana na shughuli zake za kisiasa, "ikiwemo kubuni makundi ya watu kumi kumi kusababisha vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi."
Duru ya mwisho ya kampeni za wagombea urais watatu, Rais Museveni, Dk. Besigye na Amama Mbabazi, itakuwa jijini Kampala, huku serikali ikisema itafanya kila iwezalo kuhakikisha kampeni hizo zinafanyika katika mazingira ya amani na utulivu na kwamba itakabiliana na jaribio lolote la kusababisha vurugu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages