Breaking News

Your Ad Spot

Feb 2, 2016

MFANYAKAZI WA MAELEZO AFA KATIKA AJALI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI,UTAMADUNI ,SANAA NA MICHEZO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MTUMISHI WA WIZARA YA HABARI AFARIKI  KWA AJALI YA GARI.
Kufuatia kifo cha Mfanyakazi wa  Bodi ya Filamu Tanzania Bwana Jovitha Dellan, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel ameitumia salamu za Rambirambi familia ya Mzee Dellan Tarmo kufuatia kifo kijana wao mpendwa kilichotokea juzi (tarehe 31.1.2016)kwa ajali ya gari mkoani Arusha.
“Pokea rambirambi zangu za dhati, sote kwa pamoja tumepoteza kijana  mchapakazi, hodari na aliyependa kushirikiana na wenzake katika kazi zake, hakika tutamkumbuka siku zote” Katibu Mkuu amesema.
Katibu Mkuu, Pia amemtumia salamu za pole kwa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu(KBF) na Wafanyakazi wote wa Bodi ya  Filamu Tanzania.
“Nimepokea taarifa za kifo cha Jovitha Dellan kwa huzuni kubwa, najua machungu na maumivu mliyonayo kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika utendaji wenu, poleni sana,  niko nanyi katika msiba huu mzito kwenu”, amesema Katibu Mkuu huyo.
Katibu Mkuu amesema pamoja na kwamba kifo hakiepukiki, bado ni kitu ambacho kinashtua, kuhuzunisha na kuleta unyonge mkubwa kwa wafiwa katika jamii.
 “Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu kumuombea kijana wetu Jovitha Dellan ili mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema ya Milele” Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape uvumilivu na subira katika kipindi hiki”.
“Niko nanyi katika kipindi hiki kigumu kwa hali na mali, nawaomba msijisikie wapweke” Katibu Mkuu amesema na kuwatakia utulivu na amani katika kipindi hiki cha msiba mkubwa kwa familia.
Marehemu Jovitha Dellan  amefariki juzi tarehe 31 Januari, 2016 mkoani Arusha ambapo alikuwa njiani kurejea kazini jijini Dar es salaam.
          Marehemu Jovitha Dellan anatarajiwa kuzikwa wiki hii mkoani Manyara .
          Mungu ailaze Roho ya Marehemu Jovitha Dellan mahali Pema Peponi, Amina.
Mwisho
Imetolewa na:
Idara ya Habari(MAELEZO)
DSM.
2 Februari, 2016

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages