Breaking News

Your Ad Spot

Feb 29, 2016

TAS NA UTSS WAMTAFUTA MWENZAO ALIYEPOTEA.

2 (1) 
Jacquiline Mrisho – MAELEZO. Dar es Salaam.
Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) wameiomba Serikali kuwasaidia kumtafuta Bw. Said Abdalah Ismail (47) mkazi wa Kijiji cha Mbezi Mlungwana Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa (TAS) Josephat Torner alipokua akiongea na waandishi wa habari juu ya  taarifa hii ya kupotelewa na mwenzao.
“TAS kwa kushirikiana na Shirika la Under The Same Sun (UTSS) tunaendelea kufanya juhudi ya kumtafuta na juhidi zetu tunaomba Serikali ituunge mkono” alisema Torner
Torner aliongeza kuwa, Said alionekana kwa mara ya mwisho  Januari 31 mwaka huu katika Kijiji cha Mtipule alikokwenda kuuza mboga za majani na baadae alionekana katika kilabu cha pombe ya kienyeji ambapo inasemekana aligombana na wenzie waliokua wakinywa pamoja kabla hajaondoka kilabuni hapo.
“Tunalitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na lile la Afrika Mashariki kujadili kwa kina tatizo hili  na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu pia vyombo vya dola kuhakikisha wakatili hao wanatafutwa, wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria  ili sisi wenye ualbino tuweze kuishi kwa amani.” Alisema Torner.
Amesema kuwa pamoja na juhudi za kumtafuta Said kuendelea taarifa ya kupotea kwake ilipelekwa kituo cha Polisi Wilaya ya Mkuranga na kupewa RB namba MKU/PE/05/2016 pia kituo kidogo cha polisi Kimanzichana kwa RB namba KIM/RB/50/2016.
 Aidha, Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ambapo jina la muuza pombe pamoja na majina ya wale aliogombana nao tayari yamewasilishwa polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Albino wilayani Mkuranga mkoani Pwani Hassan Kambangwa akizungumzia tukio amesema amelipokea kwa masikitiko makubwa na kuiomba Serikali kuwachukua hatua kali za kisheria wote waliohusika katika tukio hilo.
Kambangwa ametoa wito kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji kutafuta mbinu za kuzuia ukatili huo.
Ikumbukwe kuwa tukio hilo kwa Bw.Said Abdalah Ismail ni la pili kwa kuwa  aliwahi kupatwa na mkasa wa kukatwa kiganja cha mkono akiwa mkoani Morogoro miaka michache iliyopita.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages