Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International (AI)
limelituhumu jeshi la Sudan Kusini kwamba limefanya uhalifu wa kivita
kwa kuwakosesha pumzi kwa makusudi makumi ya raia waliorundikwa katika
kontena la kusafirisha bidhaa lililokuwa na joto kali.
Ripoti iliyotolewa jana na Amnesty International imesema kuwa,
wahusika wa uhalifu huo wa kivita, ambao ulifanyika katika uwanja wa
Kanisa Katoliki katika mji wa Leer kwenye Jimbo la Unity Oktoba
iliyopita, ni lazima wafikishwe mahakamani na kukabiliwa na mashtaka.
Ripoti hiyo imetegemea ushahidi wa makumi ya watu waliowaona wahanga hao
wakiingizwa kwenye kontena huku mikono yao ikiwa imefungwa au walioona
maiti zao zikitolewa kwenye kontena hilo.
Mashahidi wamesema walisikia sauti za wahanga hao wakilia na kupiga
mayowe kwa dhiki na kugonga kuta za kontena hilo ambalo halikuwa na
dirisha au sehemu nyingine ya kuingizia hewa. Ripoti hiyo imesisitiza
kuwa maafisa wa jeshi la Sudan Kusini walijua kwamba mahabusi hao wako
katika dhiki na wanafariki dunia lakini hawakuchukua hatua yoyote ya
kuwaokoa.
Shirika la Amnesty International limesema kuwa watu waliouawa katika
kontena hilo walikuwa wafugaji, wafanyabiashara na wanafunzi na wala
hawakuwa wapiganaji.
Mauaji hayo ya kutisha yaliripotiwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita
na kamisheni ya pamoja inayosimamia usitishaji vita nchini Sudan Kusini
(JMEC).
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva
Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake za zamani, Riek Machar
wa kabila la Nuer kwamba amehusika na jaribio la kupindua serikali
yake.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269