Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania, BoT, Profesa Beno Ndulu akieleza jambo wakati wa
uzinduzi wa mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa
huduma za fedha” (N-FEF) kwenye ukumbi wa mikutano wa benki kuu jijini Dar es Salaam.
Na
Mwandishi wetu
Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Kifedha
Tanzania (FSDT), imezindua Mwongozo wa taifa wenye lengo la kuongeza
uelewa kuhusu elimu ya mambo ya fedha kwa wananchi.
Uelimishwaji
wa wananchi kuhusu mambo ya fedha utatekelezwa kupitia “Mwongozo wa kwanza wa
kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
Gavana Prof.
Beno Ndulu ameuzindua rasmi mwongozo huu ambao utajikita katika kutatua
changamoto zilizobainishwa katika utafiti uliopima uelewa wa mambo ya fedha kwa
watu wazima nchini Tanzania. Utafiti huu unaitwa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa
mwaka 2014.
Utafiti huo
umebainisha kuwa watanzania wengi hawana elimu na ujuzi mahususi wa
masuala ya mambo ya fedha kwa ujumla, hivyo kuwanyima fursa ya kutumia huduma
za kifedha kwa faida yao.
Katika
utafiti huo imeonyeshwa kuwa upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa na
changamoto katika maeneo mengi huku zile zitolewazo kwa njia ya mitandao bado
hazikidhi matarajio ingawa zinawafikia wateja wengi kwa sasa.
Sambamba na
hilo kumekuwa na uhaba wa nyenzo na miundombinu ya kuhifadhi na kufikisha
taarifa za fedha kwa watumiaji wa huduma hizo kwa kuzingatia namna sahihi
ya kutoa taarifa, kuwaelimisha na kuwalinda.
Kutokana na
utafiti wa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014 wananchi kutoka makundi
mbalimbali katika jamii hawana ujuzi wa hesabu za kawaida ambao ndiyo
msingi mkuu katika nadharia ya masuala yahusuyo mambo ya fedha.
Elimu
msingi katika masuala ya fedha umekuwa kikwazo kwa waliowengi hasa katika
uandaaji wa bajeti, kutunza kumbukumbu ya matumizi, kupanga fedha kwa matumizi
yasiyotegemewa ama ya ziada na muhimu zaidi kutunza kiasi kwa ajili ya matumizi
ya uzeeni (baada ya kustaafu).
Inaonekana
kuwa upatikanaji wa taarifa za masuala ya fedha hutegemea zaidi vyombo vya
habari kama redio, televisheni na magazeti lakini vyombo hivi kwa sehemu kubwa,
hufikisha zaidi taarifa za biashara na masoko kuliko ambavyo vinaelimisha jamii
kuhusu matumizi na upangaji wa mapato yao.
“Haya ndiyo
masuala mahususi ambayo mwongozo huu wa taifa kuhusu elimu ya huduma
za fedha unalenga kushughulika nayo,” alisema Prof Ndulu.
Pamoja na
kuwepo ongezeko la upatikanaji wa huduma za kifedha, mpaka asilimia 58
mwaka 2013 kutoka kiwango cha asilimia 17 mwaka 2009, miongoni mwa watu wazima
nchini, bado mwongozo huu ni muhimu ili kuleta mfumo imara wa sekta ya fedha na
Zaidi sana ili kuleta ustawi wa maisha ya watanzania kwa ujumla.
Prof. Ndulu
anasema kutatua changamoto za kielimu kwa ujumla na hususan elimu ya huduma za
fedha italiwezesha taifa kuwa katika mwelekeo mzuri wa kukabiliana na umasikini
na kufikia malengo ya kukuza uchumi.
“Tunapaswa
kujiuliza: ni kwa namna gani wananchi hasa wale masikini na wasiokuwa na elimu
za kifedha za wanapambana kuendeleza biashara zao katika mazingira ya
soko huria na lenye ushindani kila uchwao” alisisitiza Prof. Ndulu.
Hivyo,
mwongozo huu utahakikisha watanzania wapata elimu sahihi na ya uhakika ya
huduma za kifedha pamoja na njia anazoweza nazo kujilinda katika ushindani huu.
Vilevile
mwongozo huu umeundwa ili kutatua changamoto za kifedha zinazohusiana na
maamuzi miongoni mwa watumiaji wa huduma hizi na kuwa jumuishi na wenye tija
kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mwongozo wa
taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha umeandaliwa kwa kujumisha washikadau
kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Unabainisha
changamoto zinazohusuana na uwezo wa kifedha ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa
uwepo wa elimu ya fedha. Pia, unatoa taratibu wakufanikisha utekelezaji wa
elimu ya fedha, na mwongozo wa kitaifa wa kuratibu elimu ya fedha nchini.
Lengo la
mwongozo wa elimu ya huduma za fedha ni kuwa na wananchi na kaya zenye uwezo
kifedha nchini.
Mtafiti na Mshauri
wa masuala ya fedha Bi. Susan Rutledge, akieleza umuhimu wa elimu ya masuala ya
fedha kuelekezwa kwa wananchi.
Gavana Ndulu akisoma kijitabu chenye maudhui ya mpango huo
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269