Breaking News

Your Ad Spot

Mar 11, 2016

MAREKANI YAENDELEZA HALI YA HATARI KUHUSIANA NA IRAN

Marekani yaendeleza hali ya hatari  kuhusiana na Iran
Rais wa Marekani amejadidisha hali ya hatari kuhusu Iran. Ikulu ya White House imetoa taarifa ikisema kuwa baada ya Barack Obama kuidhinisha tena hali ya hatari ya kitaifa kuhusu Iran, mabunge ya Kongres na Senate yatajulishwa rasmi kuhusu uamuzi huo.
Taarifa hiyo ambayo ilitolewa tarehe 9 Machi inasema: Pamoja na kuwepo mapatano ya nyuklia, baadhi ya hatua na sera za serikali ya Iran ni kinyume cha maslahi ya Marekani na hivyo Iran inahesabiwa kuwa tishio lisilo la kawaida kwa usalama wa taifa, sera za kigeni na uchumi wa Marekani. Kwa msingi huo kuna ulazima wa hali ya hatari kitaifa iendelee kuwepo kuhusu Iran na baadhi ya vikwazo dhidi yake
"Sheria ya Hali ya Hatari ya Kiuchumi Kimataifa" ilipitishwa mwaka 1977 katika Bunge la Kongress ya Marekani. Kwa mujibu wa sheria hiyo, rais wa Marekani anaweza kutangaza hali ya hatari ya kitaifa kufuatia tishio lisilo la kawaida la kigeni kwa usalama wa Marekani.
Hatua zinazochukuliwa katika fremu ya uamuzi huo ni kama vile kuzuia mabadilishano ya kibiashara, kufunga akaunti na kuzuia mali za nchi inayolengwa.
Kwa kutegemea sheria hii, mwezi Machi mwaka 1995 rais wa wakati huo wa Marekani, Bill Clinton alipasisha sheria ya hali ya hatari kuhusu Iran. Sheria hiyo hujadidishwa kila mwaka.
Hatua hii mpya ya Ikulu ya White House ni dalili ya wazi kuwa, kwa mtazamo wa Marekani, Iran bado ni tishio kwa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo tukiangazia historia ya uhasama wa Marekani katika kipindi cha zaidi ya nusu karne iliyopita, itabainika wazi kuwa Marekani ndiyo tishio kuu kwa usalama wa Iran.
Uhasama huo wa Marekani dhidi ya Iran ulianza hata kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hapa tunaweza kuashiria baadhi tu ya vitendo vya uhasama vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo ni pamoja na kupindiliwa serikali ya kisheria ya Iran mwaka 1953 katika njama ya pamoja ya Marekani na Uingereza, kuunga mkono makundi ya kigaidi, kuunga mkono uvamizi wa Saddam dhidi ya Iran na kumhimiza kutumia silaha za kemikali na hatua ya meli ya kivita ya Marekani ya kutungua kwa kombora ndege ya abiria ya Iran ikiwa na abiria 290 katika maji ya Iran katika Ghuba ya Uajemi mwaka 1988.
Baada ya kumalizika vita vya Saddam dhidi ya Iran, Marekani iliendeleza uhasama wake wa kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi sambamba na kutoa vitisho dhidi ya nchi hii ili kuizuia isisitawi kiuchumi.
Aidha katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Marekani iliibua madai yasiyo na msingi kuhusu Mapngo wa Nyuklia wa Iran na hivyo kuanzisha duru mpya ya uhasama wake. Hivi sasa pia Marekani imeendeleza uhasama huo kwa kuibua masuala kama vile wasi wasi kuhusu mpango wa makombora ya kujihami ya Iran jambo ambalo halina uhusiano hata kidogo na mapatano ya nyuklia ya Iran.
Marekani pia inatoa madai yasiyo na msingi kuwa eti Iran inaunga mkono ugaidi. Hii ni katika hali ambayo dunia inafahamu kuwa Marekani ndiyo iliyoibua kundi la kigaidi la Al Qaeda ili kufikia malengo yake haramu katika eneo. Baada ya kundi hilo kuwa tishio kwa Marekani, Washington ilitekeleza hujuma ya kijeshi dhidi ya Afganistan. Aidha kwa kusingizio cha kulinda usalama wa Iraq, Marekani iliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo na matokeo yake yamekuwa ni kuibuka kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na mamia ya makundi mengine ya kigaidi duniani. Aidha Marekani inaendeleza uungaji mkono wa nyuma ya pazia kwa makundi hayo ya kigaidi kwa kutoa msaada kwa nchi kama Saudia inayolea magaidi. Aidha kwa njia hiyo Marekani inaendeleza sera za chuki dhidi ya Iran katika eneo.
Utambulisho wa kujadidishwa hali ya hatari kuhusu Iran ni sehemu ya mkakati wa Marekani wa kuhalalisha sera zake zisizo za kimantiki na za uhasama dhidi ya Iran. Kilicho wazi ni kuwa lengo la uchochezi wa sasa wa Marekani ni kwa lengo la kufikia mkakati huo wa Washington.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages