Na Mwandishi Maalum
Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika utatuzi wa mgogoro wa Libya ameshiriki Mkutano wa Kamati ya Uandishi ya Baraza Maalum la Uandishi wa Katiba ya Libya (Constitution Drafting Assembly) unaoendelea mjini Salalah, Oman. Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yusuf bin Alawi bin Abdallah na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Kobler.
Katika Mkutano huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameelezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuona kuwa mgogoro wa Libya unapatiwa suluhisho la kudumu. Amewakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa jawabu la matatizo ya Libya ya hali ya usalama na changamoto zake liko mikononi mwao. Amewakumbusha dhamana kubwa iliyo juu yao na matarajio ya wananchi wa Libya kwa wajumbe hao kupawapatia Katiba ambayo itatoa majawabu kwa changamoto za Libya na kulinda haki na usawa kwa makundi yote.
Rais Mstaafu Kikwete pia amepongeza jitihada za Umoja wa Mataifa chini ya Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Kobler za kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Libya kupitia Mkataba wa Amani wa Libya (Libya Political Agreement) uliotiwa saini tarehe 17 Desemba, 2015 huko Shkirat, Morocco. Amehimiza wadau wa pande zote za siasa nchini Libya kutekeleza makubaliano hayo ikiwemo kuundwa kwa serikali na kusimikwa kwa serikali hiyo yalipo makao makuu ya nchi hiyo mjini Tripoli mapema iwezekanavyo.
Mwakilishi huyo wa Umoja wa Afrika amewahakikishia wajumbe hao utayari wa Umoja wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Falme za Kiarabu (Arab League) na wadau wengine wote kusaidia jitihada za wananchi wa Libya kurejesha hali ya usalama, amani na utulivu nchini Libya.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Mwakilshi wa Umoja wa Afrika akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Uandishi wa Katiba (Libyan Constitution Drafting Committee)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269