Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha mmoja
wa wanamapinduzi, Mzee Ibrahim Amani Kilichotokea jana tarehe 11 Machi,
2016 Mjini Unguja.
Mzee Ibrahim Amani ambaye aliwahi
kuwa Waziri na Mjumbe wa baraza la Mapinduzi Zanzibar, ni mmoja wa Watu
14 waliojitoa muhanga kupambana na kuuondoa utawala wa kisultani huko
Tanzania Zanzibar, na kuondoka kwake kunafanya idadi ya wanapinduzi
waliotangulia mbele za haki kufikia 13.
Katika Salamu zake, Rais Magufuli
amesema kwa mara nyingine Taifa limepoteza mtu muhimu, Mzalendo wa
kweli na ambaye daima alisimama kidete kutetea Taifa lake dhidi ya
vitendo vyenye kuleta madhara.
“Nimeguswa sana na kifo cha
Mzee Ibrahim Amani, maisha yake na nia yake ya kupigania uhuru na
uzalendo kwa taifa lake ni mambo ambayo daima tutayaenzi” Amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amemuomba Rais wa
Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kumfikishia salamu za pole kwa ndugu,
jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha Mzee Ibrahim Amani.
“Tumwombe Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Ibrahim Amani mahali pema peponi, Amina.” Amemalizia Rais Magufuli.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Machi, 2016.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269