
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro
Rodriguez akitoa hotuba katika mdahalo kuhusu wanawake na uzinduzi wa
Kundi la `HeForShe`.
Umoja wa Mataifa Wanawake (UN Women)
nchini umefanya uzinduzi wa kundi la mshikamano la Kimataifa
linalohusisha wanaume na wavulana lililo na malengo ya kuhakikisha
kunapatikana usawa wa kijinsia baina ya wanaume na wanawake ‘HeForShe’.
Akizindua kundi hilo, Mratibu Mkazi
wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo
(UNDP), Alvaro Rodriguez alisema usawa kijinsia ni haki ya kila binadamu
na kupitia kundi hilo ni wajibu wa kila mwanaume na mvulana kusaidia
kupatikana kwa usawa kwa wanaume na wanawake katika maeneo yote ambayo
yanaonekana kuwa na upendeleo kwa upande mmoja.
“Usawa wa kijinsia sio tu suala la
wanawake pekee, ni suala la haki za binadamu ambalo hutuathiri sisi
sote. Usawa wa kijinsia sio tu kuwawezesha wanawake, lakini pia huweka
huru watu kutoka katika ubaguzi uliowekwa kijamii na majukumu ya
kijinsia,” alisema Rodriguez.
Awali Balozi wa Sweden nchini,
Katarina Rangnitt alieleza kuwa usawa wa kijinsia unahusisha pia katika
kusimamia shughuli mbalimbali ikiwepo za nyumbani kwa wanaume na
wanawake kushirikiana kuzifanya kwa pamoja.
Alisema ni muhimu kwa jamii kuelewa
kuwa ni jambo lenye maana kuwepo kwa usawa wa kijinsia ili wanawake nao
waweze kusaidia shughuli za maendeleo kwa familia na taifa kwa ujumla.
“Usawa uwepo katika sehemu zote hata
kazi za nyumbani zifanyike kwa pamoja … ni muhimu kwa mama, baba na
kijana kuwepo kwa usawa wa kijinsia kwa watu wote,” alisema Bi.
Rangnitt.
Siku ya Wanawake kwa mwaka huu
kidunia imekuwa na kauli mbiu ya kimataifa isemayo ‘Dunia 50-50 Ongeza
Jitihada kwa ajili ya Usawa wa Kijinsia’ na kitaifa kaulimbiu imekuwa ni
’50-50 ifikapo 2030 Tuongeze Jitihada’.


No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269