Shirika la Afya Duniani WHO limepeleka timu ya wataalamu Kusini mwa
mkoa wa Nzérékoré nchini Guinea Conakry baada ya visa vipya viwili
vya Ebola kubainika na kuthibitishwa katika maeneo ya kijijini.
Maafisa wa afya wa Guinea walitoa taarifa kwa WHO na wadau wake
Machi 16 kwamba kuna vifo vitatu vinavyotatanisha katika wiki za
karibuni kwenye kijiji cha Koropara na watu wengine wa familia hizo
hivi sasa wana dalili zinazofanana na Ebola.
Wizara ya afya ya Guinea, WHO, kitengo cha Marekani cha kudhibiti
magonjwa CDC na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani
UNICEF, wamepeleka wachunguzi Machi 17, na vipimo vikachukuliwa kutoka
kwa watu wanne, na mama na mwanae wa miaka mitano ambao ni ndugu wa
mmoja wa waliokufa wamethibitishwa kuwa na virusi vya Ebola na
wamepelekwa kwenye kituo cha tiba.
Visa hivyo vipya vimethibitishwa Ijumaa, siku ambayo WHO imetangaza
kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Sierra
Leone. Shirika hilo linaonya kwamba kulipuka upya kwa ugonjwa huo
kutarajiwe, na nchi tatu zilizoathirika awali an kwamba ziwe makini na
uwezo wa kuzuia, kubaini na kukabiliana na mlipuko.
Ebola imeua zaidi ya watu 11,300 tangu mwezi Desemba 2013 katika
mripuko mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa wa ugonjwa huo uliozikumba zaidi
nchi tatu za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Inaelezwa kuwa, maradhi ya Ebola yamezorotesha pakubwa pia uchumi wa
nchi hizo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269