Breaking News

Your Ad Spot

Apr 15, 2016

SHUGHULI MBALIMBALI ZA RAIS MSTAAFU DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE JIJINI WASHINGTON D.C

Rais Mstaafu  Jakaya Kikwete akiwasilisha uzoefu wake kuhusu yatokanayo na Ripoti ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kushauri Namna Bora ya Dunia Kukabiliana na Majanga

Rais Mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete akichangia mada katika mjadala. Kulia kwake ni Bw. Stanley Bergman, CEO wa Henry Schein Inc, Bi. Ertharin Cousin, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP na Muongoza Mada Steve Stenberg

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Kamisheni na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mheshimiwa Gordon Brown na Kamishna mwenzake Bw. Anthony Lake, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF


Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ameshirikia katika Kongamano la Kimataifa la Afya lijulikanalo kama World Health Congress  lililofanyika jijini Washington D.C. tarehe 12 Machi, 2016. Katika Kongamano hilo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa ni mmoja wa Wanajopo katika mjadala unaohusu Mbinu Bora za Kukabiliana na Majanga ya Afya.



Katika mjadala huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alielezea uzoefu ambao Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kutafuta Namna Bora ya Kukabiliana na Majanga ilioupata katika nchi zilizoathiriwa na janga la Ugonjwa wa Ebola. Alieleza kuwa dunia iko katika hatari kubwa ya kuathiriwa na majanga ya afya kutokana na kuweko na mfumo dhaifu wa sekta ya afya katika nchi zinazoendelea. 


Alisisitiza umuhimu wa nchi zilizoendelea kusaidia nchi znazoendelea kuimarisha mifumo ya afya ikiwemo kujenga uwezo wa wataalam wa afya na namna ya kukabiliana na milipuko. Aidha, ameelezea umuhimu wa kupitia upya muundo na mifumo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuliwezesha kukabiliana na majanga kwa wakati ambako kwa sasa uwezo wake huo ni mdogo, na unategemea zaidi msaada na utayari wa nchi wanachama. .


Dkt Kikwete amesisitiza pia umuhimu wa dunia kuwekeza katika utafiti na ugunduzi wa kinga dhidi ya magonjwa haswa yale yanayokabili nchi masikini. Kwa ajili hiyo, Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Majanga imeshauri kuanzishwe mfuko maalum wa fedha za kwa ajili ya kuchochea utafiti na utengenezaji wa chanjo za magonjwa hayo.


Katika hatua nyingine, Rais Mstaafu jana tarehe 13 Aprili ameshiriki Mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Kushauri Namna Bora ya Kugharamia Fursa ya Elimu kwa Wote Duniani inayoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mheshimiwa Gordon Brown. 



Tume hiyo inayotegemewa kuwasilisha Ripoti yake mwezi Septemba, 2016 ina lengo la kutafuta namna bora ya kuondoa tofauti iliyopo katika viwango vya elimu duniani ifikapo mwaka 2040.  Azma ya Kamisheni hiyo ni kufikia usawa katika elimu ambapo ifikapo mwaka 2040, mtoto atakayesoma shule kutoka nchi yoyote alipo duniani apate elimu yenye ubora  unaolingana na wenzake kote duniani. 


Azma hiyo inatokana na uhalisia kuwa kwa kasi iliyopo sasa, itazichukua nchi zinazoendelea miaka 65 kufikia viwango vya elimu vya sasa vya  nchi zinazoendelea. Kwa kuanzia, Kamisheni inakusudia kupendekeza mapinduzi ya kifikra yatakayowezesha watoto wote wanaosoma katika nchi zinazoendelea  wafikie viwango vya ubora wa elimu wa nchi za uchumi wa kati ifikapo mwaka 2030 na wale wa nchi za uchumi wa kati wafikie viwango vya ubora wa elimu wa nchi zilizoendelea ifikapo 2030. 


Rais Mstaafu Kikwete aliteuliwa kuwa Kamishina wa Kamisheni hiyo kutokana na uzoefu na mchango wake katika kupanua fursa za elimu katika kipindi chake cha miaka 10 ya uongozi wake. Mkutano ujao na wa mwisho wa Kamisheni hiyo utafanyika Oslo, Norway mwezi Julai, 2016.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages