Breaking News

Your Ad Spot

May 10, 2016

JK ATEMBELEA DARAJA LA NYERERE, KIGAMBONI DAR ES SALAAM, LEO

NA BASHIR NKOROMO
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, leo amekagua Daraja la Nyerere, Kigamboni, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuona mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM. 

Baada ya kuwasili kwenye daraja hilo, Dk. Kikwete akifuatana na Mkewe Mama Salma, alipokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Joseph Nyamhanga, na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambapo mwanzoni alikagua miundombinu na kisha kutembea kwa miguu kwenye daraja hilo, huku Katibu Mkuu huyo akimpatia maelezo mbalimbali kuhusu daraja hilo.

Nyamhanga alimwabia Dk. Kikwete kwamba  Mei 14, mwaka huu, serikali itaanza kutoza tozo kwa vyombo vya usafiri vitakavyopita katika daraja hilo la Nyerere kwa lengo la kufidia gharama za matunzo na usimamizi wa endeshaji wa huduma za daraja hilo.

“ Baada ya kufunguliwa kwa daraja hili na kuanza kutumika kwa kupita bila kulipa kwa vyombo vya usafiri  tangu Aprili 19  2016 na sasa tunaanza rasmi kutoza tozo kwa ajili ya kukusanya gharama za usimamizi, utunzaji na uendeshaji wa daraja hili.” alisema Nyamhanga.

Nyamhanga alimwambia Dk. Kikwete kwamba watembea kwa miguu watapita bure katika daraja hilo huku wenye baiskeli wakilipia Sh. 300, pikipiki Sh. 600, waendesha maguta, bajaji na magari ya kawaida (Saloon Cars) watatakiwa kulipia Sh.1500.Mabasi yanayobeba  abiria 15 yatalipia  Sh. 3,000, yale ya abiria zaidi ya 15  Sh. 5,000  na yale yanayobeba  abiria zaidi  ya 29 yatalipia Sh. 7,000.

Aidha magari yenye tani zaidi ya mbili mpaka saba yatalipia Sh. 7,000, tani 7 hadi 15 watalipa Sh.10,000, tani 15 mpaka 20 watalipa Sh.15,000  na yale yenye  tani 20 mpaka 30 yatalipia Sh. 20,000.

Nyamhanga aliongeza kwamba kuwa magari yenye namba za Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi (PT), Jeshi la Magereza (MT), magari yakubeba wagonjwa, magari ya zimamoto na magari yenye vibali maalum yataruhusiwa kupita bure.

Daraja hilo la Nyerere, ambalo awali lilifahamika kwa jina la Daraja la Kigamboni, limejengwa wakati Dk. Kikwete akiwa katika awamu ya mwisho ya uongozi wake wa Urais, na lilizinduliwa hivi karibuni na Rais Dk. John Magufuli na kulipa daraja hilo jina la Nyerere.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages