Breaking News

Your Ad Spot

May 19, 2016

MALKIA WA UINGEREZA AKOSOLEWA KWA KUSHIRIKIANA NA MFALME WA BAHRAIN

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yamemjia juu Malkia Elizabeth II wa Uingereza kwa kumualika Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al-Khalifa katika sherehe za kuadhimisha miaka 90 ya kuzaliwa kwake, licha ya kufahamu dhulma na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Manama dhidi ya wananchi.
Nicholas McGeehan, Mtafiti wa Shirika la Human Rights Watch katika eneo la Ghuba ya Uajemi amekosoa namna Mfalme wa Bahrain alivyokuwa ameketi pambizoni mwa Malkia wa Uingereza katika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Malkia huyo, katika uwanja wa Windsor mjini Berkshire, kulikofanyika mashindano ya farasi yanayopendwa na Malkia huyo. Amesema ni jambo la fedheha namna Uingereza inavyodhihirisha wazi wazi juu ya uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na utawala dhalimu wa Bahrain, licha ya kufanya ukandamizaji na umwagaji damu.
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International na mashirika mengine ya kutetea haki za binaadamu, yamekuwa yakikosoa kimya cha Umoja wa Mataifa mbele ya ukandamizaji mkubwa unaofanywa na utawala wa Manama. Shirika la Human Rights Watch lilitoa ripoti hivi karibuni na kusema kuwa, mfumo wa mahakama nchini Bahrain ni wa kidhulma, kiukandamizaji na usiokuwa huru.
Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq karibuni hivi kilitoa ripoti iliyosema kuwa, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekamata watu 1,765 wakiwemo watoto wadogo 120 tokea mwaka jana 2015 hadi sasa, kwa lengo la kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga dhulma za utawala wa Manama.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages