Breaking News

Your Ad Spot

May 3, 2016

MTOTO WA MIEZI SITA APATIKANA HAI NAIROBI BAADA YA KUKAA SIKU TATU KATIKA JENGO LILILOPOROMOKA



Habari kutoka Kenya zinasema kuwa, mtoto wa miezi sita amepatikana akiwa hai bila kujeruhiwa kwenye vifusi vye jengo lililoporomoka katika mtaa wa Huruma jijini Nairobi siku tatu zilizopita.


Shirika la Msalaba Mwekundu ambalo linaongoza shughuli za uokoaji na kufukua vifusi vya jengo hilo limesema kuwa: "Mtoto huyo wa kike amepatikana akiwa hai huku amefunikwa na blanketi, zaidi ya masaa 80 baada ya jumba hilo la ghorofa 6 kuporomoka kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo".

Madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta wamesema mtoto huyo kwa jina Dealeryn Saisi Wasike anaendelea kupata nafuu ingawa walipompokea alionekana dhaifu kutokana na kuishiwa na maji mwilini.

Hadi sasa watu 21 wamethibitishwa kupoteza maisha katika mkasa huo wa Ijumaa huku wengine 139 wakiokolewa. Timu za waokoaji zikiongozwa na shirika la Msalaba Mwekundu zinasema watu 65 hawajulikani waliko na kwamba yamkini wamezikwa katika vifusi vya jengo hilo.

Huku hayo yakijiri, ndugu wawili wanaodaiwa kuwa wamiliki wa jengo hilo wamepandishwa kizimbani kuhusiana na tukio hilo na kukana mashtaka ya kusababisha vifo. Samuel Kamau Karanja & Henry Muiruri Karanja wamejitetea mahakamani hapo kuwa, wa kulaumiwa ni wahandisi waliosimamaia ujenzi huo pamoja na maafisa wa Baraza la Jiji walioidhinisha ujenzi huo.

Mahakama hiyo imeagiza kuwa wawili hao waendelee kuwekwa rumande kwa muda wa siku 21 ili uchunguzi wa kina ufanyike.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages