Na Mwandishi
Maalum
Umoja wa
Mataifa umeipongeza Tanzania kwa namna
ambavyo imechukua hatua za haraka za kukabiliana na tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia zinazowahusisha
baadhi ya walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni ya Kulinda Amani
katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(
DRC).
“Tanzania imeweza ndani ya siku tano tangu kupokea tuhuma dhidi
ya walinzi wake wa amani kuunda timu
ya kitaifa ya uchunguzi kwajili ya kuzifanyika kazi tuhuma hizo. Hatua hii na utashi ulioonyeshwa na Tanzania
ni hatua nzuri na inayopashwa kupongezwa na inaonyesha namna gani inavyochukulia
kwa uzito wa hali juu tuhuma hizo”.
Pongezi
hizo zimetolewa mwishoni wa wiki ( Ijumaa) na Bw. Atul
Khare, Naibu Katibu Mkuu Mwandamizi anayeongoza Idara ya Field Support katika Umoja wa Mataifa.
Mwishoni mwa wiki ,
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,
aliandaa mkutano ambao ulikuwa na
lengo la kutoa taarifa ya maendeleo
na mwelekeo wa Umoja wa Mataifa katika
kukabiliana na tuhuma za udhalilishaji
wa kijinsia zinazowakabili walinzi wa
Amani wa Umoja wa Mataifa, walinzi wa
Amani wa Kimataifa, na wafanyakazi raia.
Katika taarifa yake,Bw. Khare amesema, utaratibu uliopo
unaitaka nchi ambayo walinzi wake wametuhumiwa kujihusisha na vitendo vya
udhalilishaji pamoja na hatua nyingine,
kuunda timu yake ya kitaifa ya uchunguzi
ndani ya siku kumi, lakini Tanzania
iliunda timu hiyo ndani ya siku
tano na kuanza kazi jambo ambalo
amesisitiza linapashwa kuigwa na nchi nyingine.
Akabainisha
kwamba kinachosubiriwa sasa kutoka
Tanzania ni taarifa rasmi ya
kukamilishwa kwa uchunguzi huo na hatua ambazo zitakuwa zimechukuliwa kwa
walinzi ambao watakuwa wamethibitika kujihusisha na vitendo hivyo.
Tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia
dhidi ya baadhi ya walinzi hao wa
Amani wa Tanzania ziliibuliwa na Umoja
wa Mataifa mwezi March mwaka huu.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,
Balozi Tuvako Manongi, amesema utovu wa
nidhamu uliofanywa na walinzi wachache
hauwezi kuchafua kazi nzuri na sifa ya
kutukuka ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika
Misheni mbalimbali za kulinda Amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Akasema Balozi, ni kwa kutambua kazi hiyo ya kutukuka na ambayo pia imepelekea baadhi ya wanajeshi wa Tanzania kupoteza
maisha yao kishujaa wakati wakiwasaidia wananchi wa mataifa mengine kuwa na amani.
Tanzania inalichukulia kwa uzito wa kipekee
tuhuma za udhalilishaji wa
kijinsia na kwamba wale wote wataokabainika hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za
nchi.
Akaongeza kwamba
Tanzania imeamua kuwaalika wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa kwenda nchini
Tanzania ambapo watashirikiana na
wakufunzi wa JWTZ katika kuimarisha mitaala ya ufundishaji inayohusiana na masuala ya ulinzi wa raia hususani eneo la
udhalilishaji wa kijinsia.
Vilevile
Balozi Manongi amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba vitendo hivyo viovu dhidi ya raia wasiokuwa na hatia vinakomeshwa
ili pamoja na mambo mengine kurejesha
heshima ya Umoja wa Mataifa na heshima
ya nchi zinachochangia wanajeshi na polisi katika misheni za kulinda Amani.
Lakini kubwa zaidi kurejesha imani kwa
wananchi wanaohitaji ulinzi.
Akielezea
kwa ujumla kuhusu kadhia hiyo ya udhalilishaji wa kijinsi, Bw. Khare amesema,
nchi nyingine zinazochangia walinzi wa Amani na ambazo pia walinzi wao wametuhumiwa zinaendelea
ushirikiano kwa kuchukua hatua
mbalimbali ingawa pia zipo zinazosuasua.
Nchi ambazo zimetoa ushirikiano ukiacha
Tanzania ni Afrika ya Kusini, DRC, Misri na Bangladesh.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwafikisha katika mahakama za kijeshi wale
wanaokutwa na hatia, kufungwa, kufukuzwa
kazi na kutoshiriki kabisa katika misheni za
kulinda Amani na kutoa misaada kwa
wahanga.
Akaongeza
pia kwamba nchi nyingi zimeimarisha mitaala ya ufundishaji kwa
walinzi wa amani, kuandaa timu za
uchunguzi ambazo zinakuwa tayari wakati wowote zitakapohitajika, huku nyingine zikihakikisha kwamba zinakuwa na
wataalamu wa masuala
ya sheria miongoni mwa walinzi wa
Amani.
Bw. Khare
amesisitiza Umoja wa Mataifa unatambua mchango mkubwa wa walinzi wa Amani
pamoja na mazingira magumu ya utekelezaji wa mamlaka yao. Hata hivyo anasema vitendo vya udhalilishaji
wa kijinsia havipashwi kuvumiliwa wala kufumbiwa macho na kwamba kila nchi inaowajibu wa kuwafikisha
mbele ya mkono wa sheria watuhumiwa
wanaothibitika kuhusika na ukatili huo na kwamba ushirikiano na misaada kwa waathirika ni jambo la muhimu sana.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269