Kwa mara nyingine tena, Bunge la Afrika
Kusini limegeuka na kuwa ukumbi wa mieleka na malumbano kufuatia hatua
ya wabunge wa upinzani kuzusha fujo kwa lengo la kuzuia hotuba ya Rais
Jacob Zuma wa nchi hiyo.
Maafisa wa kusimamia usalama Bungeni wamewatoa nje kwa nguvu
wabunge wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters
kinachoongozwa na Julius Malema, kinara wa upinzani na mkosoaji mkubwa
wa serikali ya Rais Zuma.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa nje, Malema
amesema Rais Zuma amepoteza haiba na itibari ya kuwa kiongozi wa nchi
hiyo na kwa msingi huo, hawatamruhusu alihutubie bunge hilo kwa amani.
Ameongeza na hapa tunanukuu: "Zuma hatawahi kupata amani katika Bunge
hili, hatuwezi kuongozwa na mtu ambaye ameshindwa kutii, kutetea na
kulinda katiba ya nchi."Mwisho wa kunuku.
Itakumbukwa kuwa, mapema mwezi huu, wabunge wa upinzani walizusha
vurumai Bungeni kwa shabaha ya kuzuia hotuba ya Rais Jacob Zuma juu ya
bajeti. Floyd Shivambu, Naibu Rais wa chama hicho aliliambia bunge hilo
chini ya kiwingu cha vurumai kuwa: "Hatuwezi kumruhusu rais
anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi kuhutubia taifa kana kwamba hakuna
chochote kilichofanyika."
Wapinzani nchini Afrika Kusini wanamtuhumu Zuma kuwa ni kiongozi
fisadi, haswa baada ya Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kumpata na hatia
ya kukiuka katiba na kumuagiza kulipa sehemu ya fedha zilizotumiwa
katika ukarabati wa nyumba yake binafsi katika eneo la KwaZulu Natal,
mradi ambao uligharimu zaidi ya dola milioni 16 za Marekani. Hata hivyo
Rais Zuma alinusurika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni kufuatia
kashfa hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269