Breaking News

Your Ad Spot

May 17, 2016

PAPA FRANCIS AZIKOSOA NCHI ZA MAGHARIBI KWA KUZILAZIMISHIA NCHI ZINGINE DEMOKRASIA YAO

Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amezikosoa nchi za Magharibi kwa kulazimisha mfumo wao wa demokrasia kufanya kazi katika nchi zingine kama vile Libya na Iraq.
Katika mahojiano na La Croix, gazeti la Kanisa Katoliki la Roma la Ufaransa, Papa Francis amezikashifu nchi hizo za kibeberu kwa kushinikiza mfumo huo pasina kujali mifumo ya kitamaduni na kisiasa ya nchi hizo.
Amesema hakuna hatua zozote za maana zinaweza kupigwa katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazozikabili nchi hizo bila kuzingatia mifumo ya kijamii ya nchi hizo. Akiashiria mfano wa Libya, Papa Francis amesema nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika ilikua na 'Gaddafi mmoja', lakini sasa ina "Magaddafi 50'. Kanali Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya aliuawa mwaka 2011.
Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani amepongeza hatua ya kuchaguliwa Meya Muislamu mjini London nchini Uingereza na kusema kuwa, wakati umefika kwa nchi za Ulaya kutangamana na kuamiliana vizuri na wahamiaji. Sadiq Khan, Mwingereza mwenye asili ya Pakistan hivi karibuni alichaguliwa kuwa Meya wa Jiji la London na hivyo kuwa Meya wa kwanza Muislamu kuuongoza mji huo mkubwa katika ulimwengu wa Magharibi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages