Wakuu wa vyombo vya usalama na viongozi wa
Kiislamu wa Rwanda wamefanya mkutano katika msikiti mmoja nchini humo
kujadili mustakabali wa kiusalama.
Viongozi wa Kiislamu waliohudhuria mkutano huo uliofanyika
katika msikiti mmoja wa wilaya ya Ruhango wameelezea juu ya utayarifu
wao wa kushirikiana na vyombo vya usalama nchini humo, kwa lengo la
kuboresha usalama wa eneo hilo na nchi nzima kwa ujumla. Sheikh Ismail
Ntawukuriryayo, Imamu wa Msikiti wa Ruhango amesema jamii ya Waislamu
nchini humo inathamini usalama na amani ya nchi na kwamba daima imekuwa
ikionyesha utayarifu wake wa kuzidi kushirikiana na vyombo vya usalama
juu ya suala hilo.
Ameongeza kuwa, na hapa tunamnukuu: "Yale yote tuliyojifunza kwenye
mkutano huu wa pamoja na vyombo vya usalama, tutayapeleka katika
misikiti mingine kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii ya Waislamu wa
Rwanda inafahamu kuwa jukumu la usalama sio tu la vyombo vya usalama,
bali linahusu kila mmoja." Mwisho wa kunukuu.
Kwa upande wake, Francis Nkwaya, Naibu Kamishna wa Polisi katika Mkoa
wa Kusini amepongeza Waislamu wa wilaya ya Ruhango kwa kuwa wenyeji wa
mkutano huo na kuwataka viongozi wa dini hiyo waendelee na moyo huohuo.
Amewataka wazidi kuwahamasisha wafuasi wa dini hiyo tukufu juu ya
umuhimu wa usalama akisisitiza kuwa, wafuasi wa kila dini nchini humo
wamekuwa wakitekeleza wajibu wao wa kufanya ibada kwa miaka 22 bila
tashuwishi kutokana na usalama huo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269