Breaking News

Your Ad Spot

Jun 14, 2016

MREMA AWASHUKIA WANASIASA WANAOMKWAZA RAIS DK. MAFUGULI, AWATAKA WAMUACHE ACHAPE KAZI

Na Bashir Nkoromo
MWANASIASA mkongwe nchini na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Agostine Mrema amewataka wapinzani kumwacha Rais Dk. John Magufuli afanye kazi yake kwa kuwa amechaguliwa kihalali na bado hajamaliza hata kipindi cha kwanza cha uongozi wake.

Amewatahadharisha wananchi kuwa makini na wanasiasa kwa kuwa wapo baadhi wasio na nia njema na nchi badala yake wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi hata kama nchi inaweza kuingia kwenye majanga.

Pia amevitaka vyombo vinavyohusika na uratibu wa mambo ya siasa nchini hususan Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwatazama kwa macho mawili viongozi wa dini wanaotumia nyumba za dini kuwa majukwaa ya kisiasa huku wakiwayumbisha wananchi kwenye haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Aidha, ametaja sababu iliyomfanya ashindwe kulichukua jimbo la Vunjo ambapo pamoja na mambo mengine ni pamoja na hatua ya Rais Magufuli kumpigia debe jimboni humo jambo lililowafanya wamwonee donge na kuhamishia kampeni katika jimbo ili kuhakikisha halipati.

Hayo aliyasemwa jana mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam, alipokuwa akizungumzia hali ya kisiasa ya hapa nchini, ambapo alisema analaani kitendo cha wapinzani kudai Rais Magufuli hawatendei haki wananchi, anavunja sheria, katiba na anakiuka haki za binadamu na kuua demokrasia ya nchi.

Mrema alisema hivi sasa nchini kumeibuka vuguvugu la kisiasa hususan kwa wapinzani kutangaza serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. Magufuli imekuwa ikikiuka haki za binadamu na kuponda demokrasia jambo ambalo si la kweli kwa kuwa kila mwanasiasa yupo huru kuzungumza na kuchangia maendeleo kwa kadri anavyoweza.

Alisema wapo wanasiasa wanaodai Rais Magufuli hawatendei haki wananchi, anavunja sheria na kukiuka haki za binadamu huku wasemao hayo ndio vinara wakuu wa kukiuka haki hizo. 

"Wapinzani wenzangu ndio vinara na waliokubuhu na vitendo vya kuaribu demokrasia nchini na kuwapotosha wananchi jinsi ya katiba inavyoenda nchini,"alisema Mrema.

Aliongeza kuwa kipindi cha uchaguzi mwaka jana, Mbunge wa Vunjo James Mbatia alikiuka sheria na maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Mrema ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Vunjo, alisema NEC na taasisi zingine zinazosimamia shughuli za kisiasa nchini zinapaswa kuwa makini na baadhi ya viongozi wa dini ambao wameacha jukumu lao kuu la kuwajenga kiroho waumini wao na kutumia vyombo vya dini kama kinga yao kwenye siasa.

"Wakati wa harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka jana wapo viongozi wa dini waliosimama kwenye nyumba za ibada na kuwahubiria wafuasi wao kwamba mwaka huu rais lazima atoke kanda ya Kaskazini na nje ya hapo hatuwezi kukubali. Maneno hayo hayapaswi kuachwa yaendelee kwa kuwa ni hatari kwa mustakabbali wa siasa na maendeleo ya demokrasi hapa nchini.

"Wananchi kuweni makini si kila mwanasiasa anayekuja mbele yenu ana nia njema na taifa hili wengine lengo lao ni kutaka nchi iingie kwenye matatizo ili wao wanufaike,"alisema.

Akizungumzia kwa nini alikosa ubunge wa vunjo kupitia uchaguzi huo, alisema hilo lilitokana na mkakati wa wapinzani wenzake ambao walimuonea donge baada ya kuungwa mkono na Rais Magufuli aliposimama jimboni humo wakati wa kampeni na kumnadi.

"Nawashangaa wapinzani wenzangu hawajui kuwa Rais Dk. Magufuli anathamini zaidi mchango wangu nilioutoa nilipokuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, jinsi nilivyokuwa nafanya kazi kwa nguvu moja kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo,"alisema.

Aidha, Mrema alisema ana uhakika endapo Dk. Magufuli atakabidhiwa uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), atamtafutia nafasi ya kumsaidia kushughulika na maendeleo ya Tanzania kwa kuwa kasi yake anaimudu na ataweza kwenda nae sawa.

Hivi karibuni vyma vya upinzani hususan vinavyounda UKAWA vbimekuwa na kampeni ya kutaka kuzunguuka nchi nzima kuishitaki serikali kwa madai imekuwa ikikandamiza haki hapa nchini.

Hata hivyo, tayari polisi imepiga marufuku mikutano, makongamano na maandamano yoyote ya kisiasa kwa kuwa yanamwelekeo wa kuwachochea wananchi kukiuka sheria za nchi na kushiriki matukio ya uvunjifu wa amani.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages