Jeshi la polisi Wilaya ya Ikungi Mkoani
Singida limemtia nguvuni Diwani wa Kata ya Iseke kwa tiketi ya Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Emmanuely
Njingu kwa kudaiwa kukwamisha
shughuli za serikali kwa kuzuia watendaji wa serikali kufanya kazi yao ikiwemo
ukusanyaji wa mapato.
Njingu ambaye alikuwa mjumbe wa kamati
ya fedha awali kabla ya kuwekwa nguvuni na jeshi la polisi alivuliwa ujumbe wa
kamati hiyo kutokana na kukiuka taratibu na makubaliano ya baraza la madiwani
jambo ambalo limepelekea kuhamishiwa katikakamati nyingine.
Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa diwani
huyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye ni Diwani wa Kata ya
Irisia Ally Juma Mwanga amesema kuwa
Diwani huyo amekamatwa kwa mujibu wa sheria hivyo yeye kama mwenyekiti hawezi
kuingilia taratibu, sheria,na kanuni za serikali.
Mwanga
amesema kuwa tarehe 19 mwezi Julai moja ya maadhimio ya kamati ya fedha na
vikao vya baraza ilikuwa ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri
lakini diwani huyo amekiuka makubaliano hayo kwa kung’oa mageti ya vizuizi vya
barabarani kwa ajili ya ukaguzi wa mazao jambo ambalo limepelekea kuzorota kwa ukusanyaji
wa mapato ya Halmashauri.
Ameongeza kuwa Mjumbe yeyote anayekiuka
maazimio wanayokubaliana na kutoa siri za kamati adhabu yake kisheriani
kupoteza sifa ya kuwa mjumbe wa kamati husika.
Amesema diwani huyo ameondoshwa katika
nafasi hiyo baada ya maridhiano ya kamati hiyo na kukubaliana kumuhamishia
katika kamati nyingine ya huduma za uchumi.
“Jambo mkishakubaliana kisheria tena
kwenye vikao vya kisheria maana yake linakuwa ni sheria hivyo kwa kiongozi
yeyote akikiuka taratibu za kisheria zinachukua mkondo wake, kanuni za
Halmashauri ni za watu wote hazichagui upande mmoja” Alisema Mwanga
Hapo jana Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu alihutubia
Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ikiwa ni mara yake ya mwanzo
kabisa tangu alipochaguliwa na Rais John
Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambapo pamoja na kuzungumzia kuwepo kwa
changemoto ya uhaba wa maabara, afya duni na miundombinu pia alizungumzia
kuhusu ukusanyaji hafifu wa mapato jambo ambalo linairudisha nyuma Halmashauri
ya Wilaya hiyo.
Bajeti ya Wilaya ya Ikungi kwa Mwaka
2013/2014 ilikuwa na Shilingi 509,701,044 namakusanyoyakeyakawa ni 338,325,000
ambapo hata hivyo mwaka ulimalizika kwa kuwa na upungufuwa shilingi 171,376,044.
Mwaka 2014/2015 ilipangwa bajeti ya
shilingi 631,455,000 lakini makusanyo yake yakawa ni shilingi 457,555,172
ambapo mwaka ulimalizika kwa kukusanya 173,899,828.
Mwaka wa bajeti 2015/2016 bajeti ya
Halmashauri iliyopangwa ilikuwa ni shilingi 1,127,030,000 makusanyo yalikuwa ni
679,283,000 ambapo hata hivyo mwaka ulimalizika kwa kwa kuwa na upungufu wa
shilingi 450,747,000 hivyo kwa miaka mitatu Halmashauri hiyo imeshindwa kufikia
malengo ya ukusanyaji.
Mwanga amesema kuwa Kutofikiwa malengo hayo
kumesababishwa na kutopewa ushirikiano watendaji katika ukusanyaji wa mapato
hii ikiwa ni kufuatia kauli za mazuio zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa.
Hata hivyo ametoa Mwito kwa viongozi wa
serikali, wanasiasa, taasisi za dini na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili
kufikia malengo ya kuifanya Ikungi kukua kiuchumi .
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269