.

HALMASHAURI YA MJI WA KIBAHA YADHAMIRIA KUOKOA MIL.516.792

Aug 3, 2016


Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kibaha, Leonard Mloe akizungumzia  juu ya makusanyo ya fedha zilizokuwa zikipotea kwenye halmashauri hiyo kutokana na kuwatumia mawakala.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha ,itaokoa sh.mil.516.792 katika mwaka wa fedha 2016/2017,zilizokuwa zikipotea katika makusanyo ya ushuru wa mchanga,machinjio na stend kutokana na udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya mawakala.

Awali halmashauri hiyo ilikuwa ikitumia mawakala kukusanya ushuru wa vyanzo hivyo vya mapato na kusababisha upotevu huo wa fedha .

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo,mjini Kibaha,mwenyekiti wa halmashauri ya Mji huo ,Leonard Mloe ,alisema aligundua kuwepo kwa udanganyifu huo hivyo kuamua kuagiza makundi ya madiwani kwenda kufuatilia.

“Baada ya kuwaagiza madiwani hao kufanya uchunguzi ndipo kulipobainika kweli kulikuwa na upotevu mkubwa wa fedha ambazo zilikuwa zikifaidisha mawakala kuliko halmashauri”alisema Mloe.

Mloe alielezea kuwa kati ya fedha hizo zitakazookolewa ni pamoja na mil.335.392 zilizokuwa zikipotea kwa mwaka kwenye ushuru wa mchanga.

Alisema katika ushuru wa mchanga walikuwa wakipokea mil.264.608 kwa mwaka ambapo baada ya kutuma madiwani waligundua watakuwa wakipata mil.600 kwa mwaka.

“Katika ushuru wa stend ,halmashauri ilikuwa ikipokea makusanyo ya sh.mil.320 kwa mwaka baada ya uchunguzi tumebaini tunapata mil.458 kwa kipindi hicho na kuokoa mil 138 zilizokuwa zikipotea”alisema Mloe.

Mloe alisema upande wa machinjio walipata mil.25 kwenye tathmini imebainika fedha halisi zinazopatikana ni mil.68.400 hivyo wameokoa mil 43.400.

Aidha mwenyekiti huyo,alieleza vyanzo vyote,vya halmashauri hiyo, vibadilike hesabu zake kuanzia sasa kwani wanahitaji mapato yanayoendana na chanzo cha mapato.

Mloe alisema
 kuanzia sasa halmashauri hiyo imeanza kutumia vibarua watakaokuwa wanakusanya ushuru wa vyanzo hivyo kwa usimamizi wa watendaji wa halmashauri badala ya mawakala ambao wamebainika sio waaminifu.

“Vibarua hawa watatumiwa ndani ya miezi mitatu na baada ya hapo watakuwa wakibadilishwa ili kuondokana na tatizo la kupotea kwa fedha”alisisitiza Mloe.

Akingumzia kuhusiana na makusanyo ya mwaka 2015/2016 ,makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Robert Machumbe,alisema halmashauri ilikisia kukusanya zaidi ya bil.31.836.942 kutokana na vyanzo vyake vya mapato mbalimbali.

Alielezea kuwa halmashauri kwa robo ya nne inayoishia mwezi juni 2016 imekusanya bil.7.370.215.637 na kufanya jumla ya mapato yaliyokwisha kukusanywa kwa kipindi cha robo zote nne kuanzia Julai-Juni 2016 kuwa zaidi ya bil.25.938 sawa na asilimia 81 ya makisio ya kipindi hicho.


Machumbe alisema halmashauri ya Mji huo imekisia kutumia zaidi ya bil.31.836  kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi wa mji huo .

Alieleza katika utekelezaji wa shughuli zake kwa robo ya nne iliyoishia juni 2016 imetumia bil.5.950.420 na kufanya jumla ya matumizi kwa julai/juni  mwaka huu kufikia bil.21.614.164 sawa na asilimia 67 ya makisio.

Mwisho

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª