Breaking News

Your Ad Spot

Aug 18, 2016

NDIKILO: VIJANA AMKENI MSITEGEMEE KUAJIRIWA TU

Evarist Ndikilo
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,amesema ni wakati wa kufanya mabadiliko kwa kundi la vijana ,kwa kujenga tabia ya kujiajili wenyewe ,pasipo kutegemea kuajiliwa maofisini jambo ambalo linawachelewesha kimaendeleo.

Aidha ametoa rai kwa baadhi ya vijana kuacha kukaa vijiweni na kucheza pool bali watumie fursa mbalimbali zinazowalenga ikiwemo kambi za vijana ,ujasiliamali na kilimo .

Aliyasema hayo , wakati akizungumza na vijana waliopo kwenye kambi ya vijana iliyopo Mkongo,wilayani Rufiji ambayo itahusisha vijana 200 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini,watakaopatiwa mafunzo ya kilimo maarifa na ujasiriamali kwa vitendo .
Mhandisi  Ndikilo alisema vijana takribani bilioni 1.2 duniani hawana kazi ambapo asilimia 80 wanatoka katika nchi za Afrika ikiwemo  Tanzania hivyo amezitaka mamlaka husika zinazosimamia mpango huo kuhakikisha kambi hiyo siyo ya majaribio bali inakuwa endelevu.
Alisema waendeshaji wa kambi hiyo wameanza vizuri kutekeleza agizo la Rais la kutaka vijana kuondoka kwenye vijiwe na kuacha kuendekeza mchezo wa pool .
“Kambi hii ni sehemu ya kuwatayarisha kinadharia na vitendo kutekeleza dhana nzima ya kuchangia katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo nchini,hivyo ni vema mkaitumia vyema”alieleza Mhandisi Ndikilo.

Hata hivyo ,mhandisi Ndikilo aliomba kusiwe na  mzaha katika kusimamia mpango huo na hataki kusikia unaishia kwa muda mfupi uwe endelevu.

Alieleza kuwa amezindua kambi hiyo akitegemea kambi ya vijana ya Mkongo itakuwa yenye tija na mfano ndani na nje ya Pwani na kwamba baada ya kuhitimu wawafuatilie vijana huko watakapokuwa wanafanya kilimo .

Kaimu mkurugenzi mkuu wa RUBADA dk. Deogratias Lwezaura alisema tayari awamu ya kwanza ya mafunzo yameanza na vijana 62 kati yake 50 wametoka Rufiji na watakuwa kambini kwa siku 10 .

Alisema baada ya hapo watarudi kwenye mashamba yao na kuwafundisha wengine ( trainers of trainers ToTs) ambapo njia hiyo itasaidia kuondoa upungufu wa maafisa wagani ndani na nje ya Rufiji.

Dk Lwezaura alisema mpango wa mafunzo hayo kwa vijana utaendeshwa ndani ya miezi 12 kuanzia mwezi huu na unalenga kuwajengea uwezo katika sekta ya kilimo cha mbogamboga,ufugaji nyuki na wanyama ikiwa ni sanjali na sungura na kuku.
Alitaja changamoto zilizopo kambini kuwa ni uhakika wa maji safi ya kunywa na kumwagilia mashambani kwani kwa sasa wanataumia ya kisima cha kijiji cha Mkongo.

Dk.Lwezaura aliiomba serikali isaidie kuvuta maji ya uhakika kutoka ziwa Rungwe,tatizo jingine ni umeme uliopo ni wa nguvu ya jua kwa baadhi ya nyumba hivyo wameomba kambi hiyo iingizwe katika mpango wa REA.

Nae mkurugenzi wa SUGECO, Revocatus Kimario alieleza zipo shule nyingi zinafundisha maarifa,sayansi,afya na mengine hivyo inahitajika elimu kwa vitendo na uwezo wa kuunganisha maarifa hayo na uhalisia wake kwa vitendo ili kujenga rasilimali watu na nguvu kazi iliyoelimika kwa maarifa,ujuzi na uwezo na kutenda.

Alisema mpango wao ni kutoa elimu ya vitendo kwa asilimia 80 na maarifa ya darasani (soft skills) asilimia 20.

Awali mwakilishi kutoka FAO ambao ndio wafadhili,Fred Kafeero alimweleza Ndikilo kuwa katika programu hiyo watatengeneza miundombinu ya umwagiliaji,umeme,vifaa na nyenzo za kufundishia .

Kafeero alisema mpaka sasa wameshasaidia upatikanaji wa vifaa vya umwagiliaji (drip irrigation) vyenye uwezo wa kumwagilia ekari tano la shamba la mafunzo na wameajiri mratibu wa mafunzo na muhudumu wa ofisi . 
Vijana 200 wanatarajiwa kunufaika katika mafunzo hayo ambapo pia mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano wa mamlaka ya uendeshaji wa bonde la mto Rufiji ( RUBADA), ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO) .

Wengine ni halmashauri ya wilaya ya Rufiji chini ya ufadhili wa shirika la chakula Duniani FAO kwa kipindi cha miaka minne.



Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages