Breaking News

Your Ad Spot

Aug 14, 2016

RAIS DK. MAGUFULI AKUNWA NA WIMBO WA 'SIZONJE' WA MRISHO MPOTO, ATEGUA FUMBO LA MASHAIRI YAKE

Rais Dk. Magufuli akimpongeza Mpoto, baada ya kuimba
wimbo wa Sizonje, juzi, Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere, Dar es Salaam. Katikati ni Kaibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana
Utunzi mahiri wa mashairi na ughani uliotukuka wa Mrisho Mpoto, umeligusa sikio la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameeleza kuwa shabiki mkubwa wa kazi za msanii huyo hususan wimbo wake ‘Sizonje’.
Akizungumza na Mpoto jana, muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Magufuli alimueleza msanii huyo kuwa anazifahamu vizuri kazi zake na kwamba anaupenda sana wimbo wake wa ‘Sizonje’ huku akichambua baadhi ya mistari iliyomo kwenye beti za wimbo huo.
Mpoto alikuwa msanii pekee aliyeongozana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es  Salaam, Paul Makonda, Wakuu wote wa Wilaya za Dar es Saalam pamoja na viongozi wengine waliofika katika uwanja huo wa ndege kumpokea Mkuu huyo wa nchi.
“Nasikiliza nyimbo zako sana, ila huu wimbo wako wa Sizonje nimeuelewa sana na nausikiliza kila siku, kwangu umekuwa kama wimbo wa taifa, mwanzoni nilipata tabu kuuelewa lakini sasa hivi… aaaah, nimeuelewa vizuri sana. Halafu Sizonje namjua, nimtaje?,” yalisikika baadhi ya maneno ya Rais Magufuli kwa Mrisho Mpoto.
Akielezea tukio hilo lililoleta msisimko wa aina yake uwanjani hapo, Mpoto alisema kuwa baada ya kumsikia Rais ameanza kuusifia wimbo wake alishtuka na kujawa na furaha ya aina yake kwani kwa msanii ni jambo la thamani kubwa kusifiwa kazi yake na Mkuu wa Nchi.
Alisema kuwa pamoja na kuusifia wimbo huo, Rais alionesha kuufahamu vizuri zaidi baada ya kuanza kuipitia baadhi ya mistari na kuahidi kumfumbulia fumbo lililofichwa kwenye wimbo huo watakapokutana tena.
“Unapopata thamani kutoka kwa Mkuu wa Nchi inaleta faraja sana," amesema Mpoto. "Kwahiyo, mheshimiwa Rais leo kuniambia kwamba yeye ni shabiki wa kazi zangu na kwamba anapenda sana wimbo wa Sizonje, na akafunguka kwa mistari ‘minane’ ya Sizonje ikiwa ni pamoja na ile inayosema ‘huyu mgeni anayepitia madirishani wakati milango ipo!’ Na akaniambia siku tukikutana ataniambia vile vyumba vitatu kwanini havifunguki,” ameongeza.
Msanii huyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini mchango wake katika sanaa kwakuwa anaamini kuthaminiwa ni hitaji kubwa la kila msanii.
“Kwakweli leo ni siku yenye furaha sana. Najisikia furaha sana. Asante sana mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Umenifanya nimekuwa na siku nzuri sana,” Mpoto amefunguka kwa furaha.
Mwaka huu mwanzoni, Mrisho Mpoto aliachia audio na video ya ‘Sizonje’ aliomshirikisha Banana Zorro ambapo kwa muda mfupi tu, wimbo huo uligeuka kuwa mkubwa na kufanya vizuri. Kutokana na ufanisi wa kazi zake, Mpoto ameendelea kukubalika akipata mikataba ya ubalozi wa mashirika na taasisi kubwa nchini ikiwa ni pamoja na mfuko wa pensheni wa PSPF.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages