Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka
akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo pichani)
kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru
kaya maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini
akifafanua jambo kwa wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo
pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango
wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
Baadhi
ya wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya
maskini TASAF III katika kijiji cha Mwamgoba Wilayani Busega,
wakiwasikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na katibu
tawala Jumanne Sagini (hawapo pichani), walipozungumza nao
kabla ya zoezi la uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa ajili ya mpango
huo.
Bw. Methesela Mrobi akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu na viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya(hawapo pichani) Bwawa dogo alilochimba
kwa kutumia fedha za ruzuku za Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, ambalo
analitumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji
Mkuu wa Wilaya ya Busega , Mhe. Tano Mwera
(katikati) na Katibu Tawala Wilaya ya Busega, Bw. Sebastian Masanja (kulia)
wakizungumza jambo kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika
wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijiji cha Mwamgoba, Wilayani
Busega (kushoto) Katibu Tawala Mkoa wa
Simiyu, Bw. Jumanne Sagini
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka
akimkabidhi fedha Bw. Methesela Mrobi wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha za
ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III ,katika
kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo.
Na Stella Kalinga (Ofisi ya Mkoa wa Simiyu)
Mkuu
wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amewataka
viongozi wa kata na vijiji kuwabaini wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya TASAF
III(PSSN) wanaojihusisha na ulevi na kuwaondoa katika orodha ya wanufaika wa
mpango huo.
Mtaka
ametoa agizo hilo wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mwamgoba
wilayani Busega katika zoezi la uhawilishaji fedha za TASAF III PSSN, ambapo
jumla ya shilingi 2,976,000 zimegawiwa kwa wanufaika 82 kijijini hapo.
Mtaka
amesema lengo la mpango wa TASAF III ni kuwatoa watanzania katika hali ya
umaskini kwa kuwapa ruzuku itakayowasadia kupata huduma muhimu ikiwa ni pamoja
huduma za afya, kuwasaidia watoto wao waweze kwenda shule lakini baadhi ya
wanufaika wamekuwa wakitumia fedha hizo kulewa badala ya kuanzisha miradi
midogo midogo kama ufugaji wa kuku, mbuzi na kondoo pamoja na kilimo ili miradi
hiyo iwasaidie kuwaongezea kipato.
“Hatuwezi
kuleta fedha tukifikiri zitawasaidia kujikwamua
katika Umaskini lakini mnashinda baa na vilabuni kulewa , wengine mnaongeza
wake, tukiwabaini mtaondolewa kwenye huu mpango” , alisema Mtaka.
Mtaka
amewataka wanufaika hao kujishugulisha na kilimo na ufugaji na kuondokana na
dhana ya kuwa watakuwa wanufaika wa
mpango huo siku zote, ambapo alieleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwatoa wananchi
katika umaskini na kuwaondolea changamoto mbalimbali kama kutoa elimu ya bila
malipo na kuanzisha Mfuko wa Huduma ya Afya Watanzania wasio na uwezo waweze
kupata matibabu kwa gharama nafuu na
akatoa wito kwa wanufaika hao kujiunga na Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii (CHF)ambao
utawasaidia wao wenyewe pamoja na wategemezi wao kupata huduma za Afya katika
Vituo vya kutolea huduma za Afya.
Aidha,
ametoa wito kwa wazazi kuwakumbusha watoto wao wajibu wa kuwatunza kwa sababu
kumekuwa na baadhi ya wazee ambao wametambuliwa kuwa ni maskini, wakati wana
watoto wenye nguvu na uwezo wa kuwasaidia lakini hawatimizi wajibu wao kuwatunza
kwa kuwapa mahitaji muhimu.
Akizungumza
baada ya kukabidhiwa fedha hizo Bibi. Christina Robert ambaye ni mnufaika wa
mpango wa TASAF amesema mpango huo umemsaidia kuondokana na kuishi katika
nyumba ya nyasi na matope na kumuwezesha kujenga nyumba ya matofali na bati.
“Naishukuru
TASAF maana imenisaidia sana, ruzuku niliyopewa mara ya kwanza ilinisaidia
kutibiwa nilipofanyiwa upasuaji, mara ya pili nilitumia tena kwenye matibabu,
mara ya tatu nilinunua kuku na bata, mara ya nne nikanunua bati nikajenga nyumba ya vyumba
viwili”, alisema Christina.
Pamoja
na kusisitiza juu ya matumizi sahihi ya fedha za ruzuku za TASAF Mtaka
amewataka wananchi wa Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuongeza juhudi
katika kilimo cha mazao ya mikunde kwa kuwa tayari Serikali ya India imekubali
kununua zaidi ya tani milioni sita ya choroko, dengu na mbaazi kutoka
Tanzania, hivyo wakati utekelezaji wa
makubaliano hayo utakapoanza wananchi walime kwa wingi mazao hayo kwa kuwa
kutakuwa na soko la uhakika.
Jumla
ya kaya 4260 zilibainishwa katika vijiji 41 vya wilaya ya Busega ambapo kaya 53
ziliondolewa katika mpango wa TASAF III PSSN baada ya uhakiki na kubaini kuwa
hazikukidhi vigezo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269