Breaking News

Your Ad Spot

Aug 25, 2016

TEMEKE YAANDAA OPERESHENI STENDI YA MBAGALA

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke  imeandaa operesheni kabambe katika stendi ya Mbagala ili kuhakikisha biashara zote zinafanyika katika maeneo yaliyotengwa na yasiyohatarisha afya ya jamii.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo hilo juu ya wafanyabiashara mbalimbali waliovamia eneo hilo na kulifanya kuwa la biashara.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nassib Mbaga na kuwataka wafanyabiashara wanaofanya biashara zao katika mazingira yasiyo rasmi kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria na taratibu.

“Tumeandaa operesheni kabambe ya kuondoa Kero zilizogundulika katika stendi ya Mbagala ili kuhakikisha kwamba biashara zote zinafanyika katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo” alisema Mbaga.

Aliongeza kwa kuwataka watu wote wanaofanya biashara bila kibali katika maeneo ya stendi hiyo waondoke kabla ya zoezi la kusafisha halijaanza na kwa wale watakaokaidi, hatua za kisheria zitachukulia dhidi yao.

Aidha Mbaga alieleza kuwa kumekuwepo na jitihada za wazi za kuiweka Halmashauri katika hali ya usafi ikiwemo kutoa elimu kwa umma pamoja na kuhamasisha wananchi kuweka mazingira katika hali ya usafi na kuzuia unywaji wa maji ya kwenye vifuko vya plastiki yajulikanayo kama viroba/Kandoro kwa kuwa  hayana viwango vya ubora.

Vilevile Halmashauri hiyo itaendelea kuwakamata wale wote wanaofanya biashara hiyo na kuteketeza mali zao kisha kuwafikisha Mahakamani au kuwalipisha faini.

Mkurugenzi huyo ameyataja maeneo matano ambayo yametengwa rasmi kwa ajili ya biashara yakiwemo soko la Toangoma, Kilamba, Makangarawe, Sigara na Kiponza ambapo maeneo hayo yana huduma zote za jamii ikiwemo vyoo bora.

Maeneo mengine yaliyotengwa na Halmashauri kwa ajili ya Masoko ni pamoja na Temeke Stereo, Vetenari Tazara, Madenge, Tandika Kuu, Tandika Kampochea, Keko Magurumbasi, Temeke Mwisho, Bulyaga, Kizuiani, Zakhem, Mbagala Rangi tatu, Kampochea Mbagala, Mtoni Mtongani, Lumo, Urassa,Feri, Maguruwe, Limboa na Kabuma.

Mkurugenzi Mbaga ametoa rai kwa wananchi wanaohitaji kupata nafasi za kufanyia biashara katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo kufanya mawasiliano na Ofisi yake ili kupatiwa maeneo rasmi kwa ajili ya shughuli hizo.

MWISHO

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages