Breaking News

Your Ad Spot

Sep 7, 2016

MAKAMU WA RAIS AWASILI MKOANI MTWARA TAYARI KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU 4

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na wananchi waliojitokeza kumsalimia aliposimama Nangurukuru, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wakati akiwa njiani kuelekea mkoa wa Mtwara ambapo atakuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.
Sehemu ya Wakazi wa Nangurukuru mkoani Lindi wakishangilia ujio wa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na wananchi waliojitokeza kumsalimia alipowasili kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambapo atakuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.

.......................................................... 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali itatuma kikosi maalum cha kukabiliana na uvuvi haramu unaoendelea katika bahari ili kudhibiti na tatizo hilo ambalo limeathiri sana mazalia ya samaki na kuchangia kupungua kwa samaki baharini.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 7-Sept-2016 wakati akisalimiana na wananchi wa Nangurukuru wilayani Kilwa mkoani Lindi ambao walijitokeza kumsalimia wakati akielekea mkoani Mtwara katika ziara yake ya kikazi ya siku NNE mkoani huo.

Makamu wa Rais amesema katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika vizuri serikali pia itatuma wataalamu wa mazingira ambao watafanya tathmini ya uharibifu wa mazingira katika bahari ili kujua uharibifu uliofanyika na kuchukua hatua ya kukabiliana na hali hiyo.

Ameeleza kuwa serikali itachukua hatua hizo ili kuinusuru bahari kwa sababu imekuwa ni chanzo kizuri ya mapato kwa wananchi kutokana na shughuli za uvuvi na shughuli nyingine zikiwemo za utalii.“Bahari yetu ndio mapato yetu, bahari yetu ndio maisha yetu tumeitumia vibaya mapato yamepungua na maisha hayawi mazuri hivyo ni muhimu tuitunze ili iendelee kutulea kwa manufaa mazuri.”

Kuhusu uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kilwa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti zinazolenga kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote.

Amesema mpango huo wa uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi nchini utaenda pamoja na utoaji wa elimu bora wa wanafunzi kote nchini chini ya mkakati wa serikali wa kutoa elimu bure kuanzia wanafunzi darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Katika ziara yake mkoani Mtwara, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kesho 8-Sep-16 atazindua jengo la ofisi za Tume ya Maadili ya Uongozi wa Umma Kanda ya Kusini na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Makamu wa Rais tayari amewasili mkoani Mtwara na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angela Kairuki.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages