Breaking News

Your Ad Spot

Sep 25, 2016

NAIBU KATIBU MKUU WA CCM, VUAI ALI VUAI AIAGIZA KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA WA MAGHARIBI

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharibi kichama imeagizwa kukagua na kusimamia vizuri utekelezaji wa ilani ya Chama ya Mwaka 2015/2020 inayotekelezwa  katika majimbo ndani ya Mkoa huo ili kujiridhisha kama zimetekelezwa kweli au la.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, wakati  akizungumza na viongozi wa Kamati  hiyo huko  Ofisi ya Mkoa  huo iliyopo Mwera Unguja.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa Majimbo  hasa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wamekuwa wakitekeleza Ilani hiyo vizuri na wengine kushindwa kufanya hivyo hali inayosababisha kuongezeka kwa changamoto zisizokuwa za lazima kwa baadhi ya wananchi.

Vuai aliwambia viongozi wa Kamati hiyo kuwa pamoja na kufanya kazi za Chama bado wana jukumu la kuwasimamia Wabunge na Wawakilishi kwa lengo la kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa kwa  wananchi majimboni.

“Msisubiri  kusikia katika vyombo vya habari au kuambiwa katika vikao  kuwa  Mbunge ama Mwakilishi Fulani kachimbisha kisima au kajenga skuli (Shule) badala yake nendeni wenyewe  mkakague kwa kina miradi hiyo ili kupata takwimu sahihi za utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kila jimbo.”, alisema Vuai.

 Alisema lengo la CCM ni kuwa na viongozi imara wanaosimamia maslahi, miongozo na maelekezo ya chama na wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa vitendo ndani ya Majimbo na Wadi.

Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ndiyo tiketi halali ya kuirejesha CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Aliwasihi viongozi kushirikiana na pendana na patakapotokea mtu amekosea watumie vikao halali vya kikatiba kusululisha kasoro hizo.

Hata hivyo aliwapongeza  viongozi wa Kamati hiyo kwa kuendelea kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya CCM na maagizo ya Chama  ambapo juhudi hizo zimesaidia kuongeza kuimarika kwa hali ya  kisiasa ndani ya Mkoa huo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages