Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon amekubaliana
na ushauri wa kuhesabiwa upya kura za uchaguzi wa hivi karibuni
uliozusha machafuko nchini humo. Hata hivyo amesema, uamuzi wa mwisho
kuhusu suala hilo umo mikononi mwa Mahakama ya Katiba ya Gabon.
Kwa upande wake, Jean Ping,
mpinzani mkuu wa Rais Ali Bongo na ambaye alikuwa mgombea wa muungano wa
vyama vya upinzani katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 27 amesema kuwa,
hana imani na majaji wa Gabon kwani wote wanadhibitiwa na Rais Ali
Bongo.
Pamoja na hayo, Jean Ping amewasilisha
mashtaka katika mahakama hiyo akitaka kuhesabiwa upya kura za mkoa wa
Houto Ogooue. Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Gabon, asilimia 99 ya
wapiga kura wa mkoa huo walishiriki kwenye uchaguzi huo na matokeo
yaliyotangazwa ya kura za mkoa huo zinaonesha kuwa Ali Bongo amepata
ushindi wa zaidi ya asilimia 95 ya kura za mkoa huo ambayo ni ngome
yake.
Tume ya taifa ya uchaguzi ya Gabon
inadai kuwa ushiriki wa wapiga kura katika mikoa mingine ya nchi hiyo ni
asilimia 60, sasa suala hilo limewatia wasiwasi mkubwa wapinzani na
kutilia shaka uwezekano wa kushiriki asilimia 99 ya wapiga kura katika
mkoa huo. Mkoa wa Houto Ogooue ni wa kabila la Tek la Rais Ali Bongo,
hivyo wachambuzi wa mambo wanasema si jambo la kushangaza kuona kuwa Ali
Bongo amepata ushindi mkubwa kwenye mkoa huo.
Hii ni kusema kuwa, majaji wa Mahakama
ya Katiba ya Gabon wana muda wa siku 15 kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu
mgogoro wa matokeo ya uchaguzi ulioikumba nchi hiyo. Wafuasi wa Jean
Ping wameonya kuwa, kupeleka mashtaka kwa Mahakama ya Katiba ambayo
majaji wake 9 ni wafuasi wa Rais Ali Bongo ni kujitia kitanzi cha
kisheria, na itakuwa ni madhara kwa wapinzani na kunaweza kushadidisha
machafuko nchini humo.
Ikumbukwe kuwa watu karibu 800 wametiwa
mbaroni kwa kuhusika na machafuko yaliyotokea hivi karibuni baada ya
kutangazwa matokeo ya uchaguzi. Wafuasi wa Jean Ping wanasema kuwa watu
baina ya 50 hadi 100 wameuawa katika machafuko, lakini duru za serikali
zinasema ni watu watatu tu waliopoteza maisha yao kwenye machafuko hayo.
Kwa kweli hali ya kiusalama huko Libreville, mji mkuu wa Gabon ni mbaya
na hali hiyo imeulazimisha Umoja wa Afrika AU kuingilia kati ili
kumaliza mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Ujumbe wa AU unaoundwa na baadhi ya
viongozi wa nchi za Afrika ukiongozwa na Rais Idris Deby wa Chad ambaye
ndiye mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja wa Afrika, ulitarajiwa kuwasili
mjini Libreville jana Ijumaa tarehe 9 Septemba, hata hivyo ujumbe huo
umeakhrisha safari yake hiyo kwa sababu zisizojulikana.
Hivi sasa kuna wasiwasi kwamba wafuasi
wa Jean Ping wataitikia mwito wake wa kufanya mgomo wa nchi nchi nzima,
na hivyo kuifanya hali kuwa tete zaidi ya ilivyo hivi sasa nchini humo.
Jambo jengine ambalo linaonekana hivi
sasa ni kuwa, tofauti na miongo ya huko nyuma, sasa hivi Ufaransa
imejizuia kuingilia mgogoro wa nchi hiyo inayozungumza lugha ya
Kifaransa. Msemaji wa serikali ya Ufaransa amesisitiza kuwa, hivi sasa
ni wakati wa mabadiliko na Ufaransa inaunga mkono uamuzi wowote
utakaochukuliwa na Umoja wa Afrika kuhusiana na Gabon.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269