Waasi
Syria wamefanya mashambulizi makubwa yakilenga kuvunja mzingiro wa mwezi
mmoja masahriki mwa Aleppo, wakati mshirika wa utawala wa Syria Urusi
ukichelea kuendelea na mashambulizi mapya ya angani katika mji huo.
Mapigano
makali, mashambulizi ya makombora na miripuko ya mabomu ya kutegwa ndani
ya magari viliutikisa mji huo wa kaskazini na kuuwa wanajeshi wa
utawala wasiopungua 18 na wapiganaji washirika, kulingana na shirika la
uagalizi wa haki za binaadamu, ambalo hata hivyo halikuweza kutoa idadi
ya vifo kwa upande wa waasi.
Mji wa
Aleppo ambao wakati mmoja ulikuwa mji mkubwa zaidi wa kiuchumi nchini
Syria, umeharibiwa na mgogoro huo ulioanza mwezi Machi 2011 kwa
maandamano ya kuipinga serikali na hadi sasa umesababisha vifo vya zaidi
ya watu 300,000. Udhibiti wa mji huo, uliogawika kati ya upande
unaodhibtiwa na waasi mashariki na magharibi ikiwa mikononi mwa vikosi
vya Assad, ni muhimu katika kurejesha udhibiti wa Syria kaskazini.
Mashambulizi
ya waasi siku ya Ijumaa yamekuja zaidi ya miezi mitatu tangu serikali
ilipoanzisha juhudi za kuyazingira maeneo ya Aleppo mashariki ambako
watu zaidi ya 250,000 wanaishi, na wiki kadhaa baada ya jeshi kuanzisha
operesheni inayonuwia kuurejesha mikononi mwake upande unaoshikiliwa na
waasi mashariki.
Makundi
ya waasi "yanatangaza kuanza kwa mapambano ya kuvunja mzingiro wa
Aleppo," alisema Abu Yusuf Muhajir, kamanda wa kijeshi na msemaji wa
kundi la Ahrar al-Sham. Mshambulizi hayo "yatakomesha ukaliaji wa
utawala katika upande wa Aleppo magharibi na kuvunja mzingiro kwa watu
waliokwama ndani," aliliambia shirika la habari la AFP.
Mapigano
yalikuwa yaliendelea hadi Ijumaa usiku magharibi na mashariki mwa
Aleppo, lakini yalipungua makali, kulingana na mwandishi wa AFP katika
maeneo ya waasi.
Jeshi la Urusi lataka kurejelea mashambulizi
Moscow
inasema haijaishambulia Aleppo tangu Oktoba 18 lakini jeshi la Urusi
lilisema siku ya Ijumaa kuwa limemuomba rais Vladmir Putin kutoa idhibi
ya mashambulizi ya angani kurejea tena. Lakini msemaji wa ikulu ya
Kremlin Dmitry Peskov alisema Putin "anaichukulia hatua hiyo kuwa
isiyofaa kwa wakati huu," na kuongeza kuwa rais huyo alidhani ni muhimu
"kuendeleza usitishaji mapigano wa kibinaadamu" katika mji huo
ulioharibiwa vibaya na vita.
Licha ya
msaada wa mashambulizi ya angani kutoka kwa Urusi, utawala wa Syria
umepata mafanikio kidogo katika jitihada zake za kuiteka Aleppo nzima.
Marekani iliutuhumu utawala huo siku ya Ijumaa kwa kutumia njaa kama
zana ya kivita -- jambo ambalo ni uhalifu wa kivita chini ya mikataba ya
Geneva -- na kuongeza ukosoaji dhidi ya Assad na waungaji wake mkono
Urusi.
Akipinga
madai ya Urusi kwamba mashambulizi dhidi ya Aleppo yamekoma, afisa wa
serikali ya Marekani aliliambia shirika la AFP "utawala umakataa maombi
ya Umoja wa Mataifa kufikisha msaada Aleppo mashariki -- ukitumia njaa
kama silaha ya kivita".
Wiki
iliyopita Urusi ilitekeleza mpango wa usitishaji mashambulizi ilioutaja
kuwa wa "kibinadamu" wenye lengo la kuwaruhusu raia na waasi
wanaojisalimisha kuondoka upande wa mashariki. Lakini ni wachache sana
waliofanya hivyo, na mpango wa Umoja wa Mataifa kuondoa majeruhi
ulishindwa kwa sababu usalama haukuweza kuhakikishwa.
Wakati
waasi wakianzisha mashambulizi yao ya kwanza makubwa, shirika la
uangalizi wa haki za bindaamu lilisema raia wasiopungua 15, akiwemo
mwanamke na watoto wawili, waliuawa, na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika
mashambulizi ya waasi Aleppo Magharibi.
Shirika
hilo liliripoti makabiliano makali katika maeneo mbalimbali katika kingo
za magharibi na kusini mwa Aleppo Magharibi, ambapo magari matatu ya
waripuaji wa kujitoa muhanga yalilenga kituo cha ukaguzi katika eneo la
Dahiyet al-Assad.
Ngome za serikali zalengwa pia
Waasi pia
walizilenga ngome za serikali mashariki mwa Aleppo na katika mkoa wa
pwani wa Latakia, kikiwemo kituo cha kijeshi cha Hmeimim kinachotumiwa
na vikosi vya Urusi vinavyousaidia utawala. Mwandishi wa shirika la AFP
Aleppo Mashariki alisema mashambulizi ya waasi yaliongeza morali huko,
ambapo misikiti ilitangaza "Allah ndiye mkubwa zaidi" kupitia vipaza
sauti.
Alisema
wakaazi walichoma matairi ili kuunda moshi na kuweka kizuwizi dhidi ya
mashambulizi ya angani. Mvua kubwa ziliuzima moto huo lakini pia
zilikwamisha operesheni za angani za jeshi la Syria, na kuunda kile
ambacho mmoja wa waasi alikitaja kuwa "ukanda mtakatifu usiyoruhusiwa
kuruka ndege."
Shirika
la uangalizi lilisema waasi pia walifyatua maroketi dhidi ya uwanja wa
ndege wa kijeshi wa Nairab na uwanja wa kimataifa wa Aleppo, vyote
vikiwa mashariki mwa mji na vinadhibitiwa na serikali. "Kuvunjwa kwa
mzingiro hakuepukiki," alisema Yasser al-Yusuf, mjumbe wa ofisi ya
kisiasa ya kundi la waasi la Nuredine al-Zinki.
Kwa
upande wake, televisheni ya serikali ilisema "jeshi limetibua njama ya
magaidi kuushambulia mji wa Aleppo kutokea pande kadhaa kwa kutumia
mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga". Shirika la habari la
serikali SANA lilisema ndege za serikali zilikuwa zinafanya mashambulizi
kusini na magharibi mwa Aleppo.
Umoja wa
Ulaya ulisema Ijumaa kuwa mwanadiplomasia wake wa juu kabisaa Federica
Mogherini alikuwa naelekea nchini Iran na Saudi Arabia kwa ajili ya
mazuungumzo kuhusu vita hivyo vya miaka mitano.
Shinikizo
hilo la kidiplomasia linakuja wakati kukiwa hakuna mataumaini ya
kukomeshwa kwa mgogoro huo ulioziweka nchi hizo kubwa kabisaa kikanda
katika pande pinzani, ambapo Iran inamuunga mkono Assad na Saudi Arabia
ikiwa muungaji mkono muhimu kwa waasi wanaopambana kumng'oa madarakani.DW
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269