.

IRAN YAMTAKA RAIS WA DJIBOUTI AACHE KUTUMIKIA AMRI ZA WENGINE

Nov 26, 2016

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti aliyedai kuwa, Tehran inaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kumtaka atatue matatizo ya nchi yake kwanza na aache kutekeleza amri anazopokea kutoka kwa watu wengine.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi alisema hayo jana na kuwataka viongozi wa Djibouti watumie hekima na waache kutoa madai yasiyo na msingi.
Amesema, ni vyema kwa Rais wa Djibouti kuacha kutoa madai ya uongo na yasiyo na msingi anayoyasikia kutoka kwa wengine, na aangalie mambo kwa uhalisia wake kwa ajili ya kuimarisha utulivu na manufaa ya wananchi wa eneo hili zima.
Qassemi amesisitiza kuwa, madai kama hayo ya Rais wa Djibouti kamwe hayawezi kusaidia kuimarisha usalama na amani ya eneo hilo, wala hayawezi kutatua migogoro ya Syria, Yemen na Bahrain.
Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amemtaka Rais wa Djibouti kusoma kwa makini historia na ustaarabu wa mataifa ya dunia hususan ya eneo hili.
Siku ya Jumatano, Rais wa Djibouti alikariri madai ya Saudi Arabia ya kwamba eti Iran inaingilia masuala ya nchi za Kiarabu kama vile Yemen, Bahrain, Syria na Iraq na kwamba eti nchi za Kiarabu zina haki za kukabiliana na uingiliaji huo wa Iran katika masuala ya eneo hili.
Itakumbukwa pia kuwa, tarehe 6 Januari mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf alisema kuwa, nchi hiyo ndogo ya Pembe ya Afrika imeamua kukata uhusiano wake na Iran ili kufuata siasa za Saudi Arabia. 

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช