.

MASHAMBULIO YA KUNDI LA KIGAIDI LA BOKO HARAM KASKAZINI MWA CAMEROON

Nov 26, 2016

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram la Nigeria limeshadidisha mashambulio yake katika miezi ya karibuni nchini Cameroon ambapo kwa mujibu wa ripoti ya kundi la kimataifa la migogoro kundi hilo limeshambulia kambi tatu za jeshi la Cameroon katika maeneo ya Darak, Diguina na Kolofata nchini humo.
Licha ya mpasuko na mgawanyiko uliojitokeza katika miezi ya karibuni ndani ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kutokana na hitilafu za ndani, mashambulio ya kigaidi ya kundi hilo yangali yanaendelea kushuhudiwa.
Mashambulio ya karibuni ya Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa Cameroon yameshadidi baada ya mamlaka za nchi hiyo kutaka kufungua tena mpaka wa pamoja wa Cameroon na Nigeria. 
Mpaka wa pamoja Cameroon na Nigeria katika maeneo ya kaskazini mwa Cameroon ulifungwa mwaka uliopita wa 2015 kutokana na kuenea na kushadidi machafuko na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Kutokana na hali hiyo hatua kali zaidi za usalama zilichukuliwa ambapo hivi sasa vikosi vya jeshi la Cameroon vimewekwa katika hali ya tahadhari kwenye eneo la Ziwa Chad.
Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram
Japokuwa ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram iko katika mji wa Maiduguri makao makuu ya jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, lakini tangu miaka mitatu iliyopita mashambulio ya kundi hilo yameenea hadi katika nchi tatu jirani na Nigeria za Cameroon, Niger na Chad.
Katika kukabiliana na kitisho cha Boko Haram cha kuhatarisha amani na uthabiti wa eneo viongozi wa nchi hizo jirani pamoja na Nigeria yenyewe waliamua kuunda kikosi cha pamoja cha askari 10,000 kukabiliana na kundi hilo.
Kuanzia mwezi Februari mwaka jana operesheni za pamoja za nchi hizo nne zilianza dhidi ya ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ambapo idadi kadhaa ya magaidi wa kundi hilo la kitakfiri wamejisalimisha kwa jeshi la Cameroon.
Wakati huohuo makamanda wa jeshi la Cameroon wamelitangazia na kulionya kundi la kigaidi la Boko Haram kwamba ima lijisalimishe au lijue kuwa mwisho wake unakaribia.
Kwa mtazamo wa wafuatiliaji wa masuala ya Afrika Magharibi viongozi wa nchi za eneo la Ziwa Chad ambazo ni Nigeria, Niger, Chad na Cameroon wameungana na wana dhamira ya kweli ya kuliangamiza kundi la Boko Haram.
Katika kikao cha 11 za Kiafrika kilichofanyika tarehe 23 mwezi huu katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger alisisitiza kwa mara nyingine tena juu ya kupambana na ugaidi katika eneo la magharibi mwa Afrika.
 Rais Mahamadou Issoufou wa Niger 
Sambamba na hayo maafisa wa usalama na intelijinsia wa Nigeria wameanzisha operesheni ya kuwasaka na kuwatokomeza watu 55 wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na Boko Haram. Ukweli ni kwamba hujuma na miripuko ya mara kwa mara inayolenga mabomba ya mafuta katika eneo lenye utajiri mkubwa wa nishati hiyo la kusini mwa Nigeria imeiweka katika hali ngumu serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo ambayo inalazimika kukabiliana na tatizo hilo sambamba na kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi.
Kwa mtazamo wa wachambuzi, operesheni zinazotekelezwa hivi sasa na jeshi la Cameroon dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram zina umuhimu mkubwa kwa sababu matunda yake yatakuwa ni kwa faida ya nchi zote za eneo.
Eneo la Bonde la Ziwa Chad
Katika miaka ya karibuni kundi la Boko Haram limekuwa tishio kubwa la ugaidi kwa Nigeria na nchi jirani katika eneo la magharibi mwa Afrika kama ambavyo kundi jingine la kigaidi la Al-Shabaab nalo pia linahatarisha amani na uthabiti wa Somalia na nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika. Katika hali kama hiyo  kuwa na msimamo na ushirikiano wa pamoja wa kieneo kati ya nchi jirani ni wenzo muhimu wa kuyashinda makundi ya kigaidi ambayo yamechipua taratibu katika maeneo tofauti ya Afrika na hivi sasa yanaendelea kushamiri na kuzagaa ndani ya bara hilo.../

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช