Taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Gallup imetangaza ongezeko la wimbi la manung'uniko ya raia wa Marekani.
Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya Gallup, asilimia 73 ya raia
wa Marekani hawakubaliani na mwenendo wa matukio yanayojiri nchini
mwao. Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la asilimia 10 la malalamiko
hayo ikilinganishwa na mwezi uliopita. Aidha takwimu hizo zinatoa ujumbe
kwamba, kati ya kila Wamarekani 10, ni Wamarekani watatu pekee ndio
wanaoridhia mazingira ya ndani nchini humo.
Kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais hapo Novemba nane mwezi huu,
kiwango cha ridhaa ya raia wa taifa hilo, kilifikia asilimia 37, kiwango
ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miongo
ya hivi karibuni. Hata hivyo, ushindi wa Donald Trump, mgombea wa chama
cha Republican, umekifanya kiwango hicho kupungua sana. Isisahulike
kuwa, manung'uniko ya raia nchini Marekani yanarejea nyuma hata kabla ya
kutangazwa matokeo ya uchaguzi uliopita. Hali mbaya ya uchumi, hususan
uhaba wa fursa mpya za ajira, ni miongoni mwa malalamiko ya raia wengi
wa nchi hiyo. Kwa kuzingatia kuwa takwimu rasmi za ukosefu wa ajira
zinaelezea kiwango cha karibu asilimia tano, hata hivyo uchunguzi huru
unaelezea ongezeko la mara mbili zaidi ya hali hiyo.
Mbali na hayo, ugawaji usio wa kimantiki wa ajira nchini Marekani
baina ya wanawake na wanaume, vijana na wazee na weupe na weusi ni
miongoni mwa malalamiko ambayo yamekuwepo kwa muda sasa nchini humo.
Katika fremu hiyo, kuibuka matatizo ya kifedha yanayokabili serikali ya
Marekani, kumesababisha kuzorota pia huduma za kijamii kama vile ulipaji
wa bima za kazi, kudhamini bima za afya za viwango vya chini, ugawaji
wa ruzuku za chakula na misaada ya masomo, sanjari na
kuzidisha mashinikizo kwa watu wa tabala la kati na masikini. Watu hao
hivi sasa wanakabiliwa na mgogoro wa ukosefu wa ajira na kupanda kwa
gharama za maisha, kama ambavyo pia wanatakiwa kubeba mzigo unaotokana
na natija ya kufeli mipango ya ustawi ya serikali.
Mbali na matatizo ya kiuchumi na kimaisha, Wamarekani wanakabiliwa
pia na migogoro ya kijamii. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni,
kiwango cha ustahamilivu wa tofauti za rangi kimezidi kushuka nchini
Marekani. Kwa upande mmoja, weupe wana wasi wasi wa kuingia katika
ushindani na watu wasio wazungu na wahajiri kwenye maisha ya kisiasa na
kiuchumi dhidi yao, huku kwa upande wa pili ubaguzi dhidi ya wasio
wazungu na wahajiri ukiwa umeshtadi zaidi nchini humo. Katika fremu
hiyo, ufyatuaji risasi wa polisi dhidi ya vijana wenye asili ya
Kiafrika, umeongeza malalamiko ya kupinga wimbi la ubaguzi nchini humo.
Ukweli ni kwamba, suala hilo na lile la mgogoro wa kiuchumi, ni mambo
ambayo kwa pamoja yanasambaratisha ndoto za Wamarekani. Katika hali
hiyo, kushindwa mfumo wa kisiasa katika kutatua matatizo ya kijamii na
kadhalika kufichuliwa kashfa za ufisadi za viongozi wa kisiasa,
kumezidisha hasira ya wananchi dhidi ya serikali. Malalamiko ya wananchi
yameongezeka kiasi cha kuwafanya wampigie kura mtu ambaye amekuwa
akikosoa vikali mfumo wa jadi wa kibepari na muundo wa kisiasa na
kiuchumi nchini humo.
Kwa kutumia wimbi la malalmiko makali ya Wamarekani, Donald Trump,
mgombea wa chama cha Republican, ameweza kuibuka mshindi katika uchaguzi
uliopita kutokana na hali hiyo. Hata hivyo uchaguzi huo nao pia
umeshadidisha tena wimbi la malalamiko ya wananchi ikilinganishwa na
kipindi cha hapo nyuma. Hii ni kwa kuwa wengi wa Wamarekani wamekumbwa
na hali ya wasi wasi juu ya ahadi alizozitoa Trump, ikiwa ni pamoja na
kuwaondoa wahajiri haramu na kupiga marufuku Waislamu kuingia nchini
hummo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269