Breaking News

Your Ad Spot

Nov 25, 2016

MUHIMBILI YAFANYA UPASUAJI MKUBWA WA KUHAMISHA MISULI

misu1
Madaktari na wataalamu wengine wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Tanzania Australia Society  na Rafiki Surgical Mission wakimfanyia upasuaji mgonjwa wa kuvuna mishipa na misuli katika mguu wake wa kulia na kupandikiza katika sehemu yenye uhutaji husika. Madaktari bingwa wa Muhimbili wanaofanya upasuaji huo ni Dk. Ibrahimu Mkoma, Dk Edwin Mrema, Dk. John Tupa na Dk Frank Muhamba ambaye anapitia mafunzo ya kuwa daktari bingwa wa upasuaji. Mwingine ni daktari bingwa wa upasuaji, James Savundra na wataalamu wenzake kutoka Australia.
misu2
Daktari Bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Edwin Mrema akizungumza na waandishi wa habari Leo katika chumba cha upasuaji ambako kumefanyika upasuaji huo.
Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili leo kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji kwa kutumia darubini (microvascular surgery) wa kuhamisha misuli na mishipa ya damu kutoka kwenye mguu kwenda sehemu nyingine chini ya mguu (free gracilis muscle transfer).
Upasuaji huu wa aina yake na ambao mara nyingi huchukua muda wa saa sita hadi saba una lengo la kujenga uwezo kwa watalaamu wa ndani ili waendelee kutoa huduma za ubingwa wa hali ya juu kwa Watanzania wengi zaidi na vilevile kupunguza kasi ya kupeleka wagonjwa nje.
 Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambaye pia ameshiriki upasuaji huo Dk Ibrahim Mkoma amesema upasuaji huo unagharimu kiasi cha dola 40,000 za Marekani nchini Australia ikiwa ni gharama ya upasuaji tu.
Lengo kubwa la ushirikiano wa upasuaji huu ni wataalamu kutoka Australia kuwaachia taaluma ya upasuaji huo madaktari MNH ili iweze kuendelea kufanya upasuaji huo mbeleni.
Aidha Dk Mkoma amesema kuwa kuanzia mwakani kutakuwa na utaratibu ambao utaanzishwa Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, wa taaluma maalumu ya kusomea upasuaji wa aina hiyo ili kuweza kupata wataalamu zaidi kutoka nchini.
Amesema hakuna chuo chochote Tanzania kinachotoa taaluma hiyo ya plastic surgery kwa sasa.
Dk Mkoma amesema MNH inajivunia kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Australia akiwapo Daktari  bingwa James Savundra ambaye ni Rais wa Madaktari Bingwa wa upasuaji kutoka timu ya upasuaji nchini Australia.
Daktari bingwa wa upasuaji kutoka Australia,  Dk James Savundra amesema upasuaji huo ni moja ya upasuaji ambao umekuwa ukifanyika kwa gharama kubwa.
“Nchini Australia mgonjwa mmoja hufanyiwa upasuaji kwa dola 130 za Marekani kwa dakika moja hiyo ikiwa ni gharama za chumba cha upasuaji ambazo ni kwa ajili ya kuwalipa madaktari wa upasuaji, madaktari wa usingizi, wauguzi na watalaamu wengine waliohusuka katika upasuaji huo,” amesema Dk Savundra.  
 Amesema gharama hiyo haijumuishi huduma nyingine ambazo mgonjwa huyo anatakiwa kupata ikiwamo  huduma ya wodini na kadhalika.
“Tumefanya upasuaji huu kwa kushirikiana na madaktari Bingwa kutoka nchini Australia kupitia mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Tanzania Australia Society na Rafiki Surgical Mission,”amesema Dk. Mkoma.
Mpaka sasa wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa aina hiyo Muhimbili ni watatu mbali na sita waliofanyiwa upasuaji mbalimbali ukiwamo upasuaji wa shavu, nyonga, mkono na ziwa.
 Mapema wiki hii, Muhimbili imeanza kambi maalumu ya upasuaji kwa wagonjwa wenye kuhitaji upasuaji maalumu kwa kushirikiana na madaktari hao kutoka nchini Australia.
Hospitali ya Taifa Muhimbili iko kwenye mageuzi makubwa katika kuboresha huduma mbalimbali ambapo Disemba mwaka huu inatarajia kuanza kutoa huduma za upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watoto  wanaozaliwa na matatizo ya usikivu. Wakati huohuo Januari mwaka 2017 Hospitali hii inatarajia kuanza kufanya upasuaji wa kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye matatizo hayo.(P.T)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages