Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa zimepasisha mpango wa kuundwa kamati ya uchunguzi kuhusiana
na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi.
Mpango huo umepasishwa katika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huku serikali ya Burundi
ikiendelea kupinga madai ya kuweko ukiukaji wa haki za binadamu nchini
humo. Miezi miwili iliyopita, wataalamu wa kujitegemea wa Umoja wa
Mataifa waliwasilisha ripoti katika Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa ikielezea kuweko vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu
nchini Burundi.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa katika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya wataalamu hao kuitembelea
Burundi, ililaani vikali kile ilichokieleza kuwa, ukiukaji mkubwa wa
haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kiafrika unaofanywa na vyombo vya
usalama.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kamati hiyo itakuwa na muhula wa mwaka
mmoja kufanya kazi yake ya kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu
nchini Burundi.
Burundi imekuwa ikishuhudia hali ya
mchafukoge tangu mwezi Aprili mwaka jana, baada ya chama tawala cha
CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea kwa
muhula wa tatu katika uchaguzi wa rais uliopita.
Kwa mujibu wa asasi za kutetea haki za
binaadamu nchini Burundi, hadi sasa kwa akali watu 450 wamekwishapoteza
maisha kufuatia machafuko hayo, huku maelfu ya wengine wakilazimika kuwa
wakimbizi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269