Na Lilian Lundo
MAELEZO
Dar es Salaam
KAMISHENI ya Ngumi za
Kulipwa nchini (TPBC) imemfungia Bondia Francis Cheka kushiriki katika mchezo wa
ngumi kwa kipindi cha miaka miwili na kulipa faini ya shilingi laki tano kwa
kitendo cha kukacha pambano baina yake na Bondia Abdallah Pazi (Dulla Mbabe).
Akizungumza na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Msaidizi wa TPBC, Chatta
Michael alisema kamisheni hiyo ilitoa kibali cha pambano kati ya Cheka na
Abdallah Pazi lakini bondia huyo hakufika katika pambano hilo huku akiwa
ameshalipwa kiasi cha shilingi milioni tatu.
Chatta alisema kuwa Cheka
aliaharisha pambano hilo lililokuwa lifanyike katika ukumbi wa Sabasaba tarehe
25 Desemba mwaka huu pasipo na kutoa taarifa, wakati Promota wa pambano hilo alikwishaingia
gharama mbalimbali za maandilizi ya pambano hilo.
“Kamisheni
imejiridhisha kuwa kiasi cha shilingi milioni tatu kilitolewa kwa Francis Cheka kabla ya pambano, hivyo
alitakiwa apatiwe kiasi kilichobaki baada ya pambano kama alivyokubali na
kusaini mkataba wa pambano hilo,” alifafanua Chatta.
Aliongeza kuwa kitendo
cha kutotii makubaliano na kuchukua fedha bila kuifanyia kazi si jambo la
kawaida kwa kuwa lina madhara makubwa katika kuendeleza mchezo wa ngumi za
kulipwa nchini.
Kwa mujibu wa Chatta
alisema TPBC imetoa adhabu hiyo ili kuwa fundisho kwa mabondia wengine ambao
wanaweza kusababisha mchezo wa ngumi kupoteza uaminifu kwa wakuzaji na
kusababishha uvunjifu wa amani kwa watazamaji iwapo wataendelea kudanganywa kuhusu
uwepo wa mapambano hewa.
Kwa upande wake, Rais
wa TPBC,Chaurembo Palasa alisema adhabu hiyo ni mwanzo wa kuboresha mchezo wa
ngumi za kulipwa kwani mchezo huo umekuwa ukiendeshwa bila kufuata sheria,
kanuni na taratibu kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269