Na.
Lilian Lundo
MAELEZO.
Dar
es Salaam
30.12.2016
Serikali kupitia Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
pamoja na Tume ya Taifa ya UNESCO
wamekusudia kuandaa tamasha na matembezi mbalimbali ili kutoa elimu kwa jamii
kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
Hayo yamebainishwa
leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Moshi Kimizi namna ambavyo Serikali imekusudia
kuanzisha kampeni hizo ili kuionyesha jamii athari mbalimbali za kisaikolojia
na kiafya kwa wachezaji na hasa vijana.
Aliongeza kuwa mwezi
Juni mwaka huu, Bunge la Tanzania liliridhia mkataba wa kimataifa wa udhibiti
wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu katika michezo, hatua iliyolenga
kulinda na kuimarisha afya za wanamichezo nchini.
“Kwa kuridhia mkataba
huu na kuutekeleza itainufaisha nchi kuweza kuhudhuria mafunzo, mikutano na
vikao vya kimataifa na kushiriki katika makongamano yenye maamuzi mbalimbali
yanayohusu suala hili” alisema Dkt. Kimizi.
Kwa mujibu wa Kimizi
alisema kupitia mkataba huo, wanamichezo, walimu wa michezo na wadau wa michezo
wataweza kuelimishwa kuhusu athali za matumizi ya dawa au mbinu za kuongeza
nguvu michezoni pamoja na aina ya vyakula au vinywaji ambavyo vina asili ya
kuongeza nguvu mwilini.
Kwa upande wake Afisa
Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Rashidi Mijuza alisema kuwa, wanamichezo wengi hujikuta wakiwekewa dawa
za kuongeza nguvu na walimu wao katika
chakula au vinywaji bila kujua ili tu waweze kushinda.
Kwa mujibu wa Mijuza
alisema Serikali imekusudia kutoa elimu kwa wanamichezo na walimu ili kuondokana
na visingizio vya kutojua au udanganyifu ambao umekuwa ukifanyika kwa
wanamichezo pindi wanapokuwa katika mashindano mbalimbali.
“Kwa Tanzania kuridhia
mkataba huo, nchi itanufaika na mambo mbalimbali katika sekta ya michezo ikiwa
ni pamoja na Tanzania kushiriki na kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa,
kupata misaada ya wataalamu, fedha na mafunzo kwa ajili ya utekelezaji wa
makubaliano” alisema Mijuza
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269