.

SIMULIZI ZAKUSISIMUA : SIKU NYEREREALIPOTUA MLIMANI, SWALI LA KWANZA LILITOKA KWA MUSEVENI..

Dec 10, 2016

Ndugu zangu,
Ikafika siku ile Julius Nyerere akaenda mwenyewe pale Mlimani kuongea na wanafunzi. Julius alikuwa makini sana.

 Aliposikia juu ya tuhuma zile kutoka kwa Vijana wa TANU dhidi ya akina Museveni na USARF yao, kwamba wanapiga kampeni dhidi ya sera za TANU, alielewa, kuwa huenda kuna ' Majungu Yanapikwa' dhidi ya USARF.

Neno USARF kirefu chake ni ' University Students Africa Revolutionary Front.
Nyerere hakutaka kukimbilia kuwahukumu USARF, bali, kwenda Mlimani, na kupitia staili yake ya kuongea na kuruhusu maswali, angepima mwenyewe.

Na ndivyo ilivyokuwa, huku USARF nao walijipanga chini ya Museveni kupanga mikakati ya siku hiyo Nyerere atakapokuja kuongea na wanafunzi.
Kuna miongoni mwa wanachama wa USARF waliofikiri, kuwa strategia nzuri ni kutouliza maswali siku hiyo Nyerere atakapokuja. Lakini, Museveni akawaambia wenzake kwenye USARF, kuwa hilo litakuwa kosa kubwa kimkakati, maana, Nyerere ataamini katika majungu aliyopelekewa na Vijana wa TANU. Tutaonekana wanafiki. Museveni akawaambia wenzake, kuwa ni lazima waandae maswali.
Kulikuwa na utaratibu wa maswali kupelekwa kwa Makamu Mkuu wa Chuo kabla siku ya tukio. Museveni akawa na swali lake pia. Akalipeleka.
Jambo lingine, ni kuwa,  kutokana na USARF kuonekana ni wenye kuwakosoa sana wahadhiri pale Mlimani. Baadhi ya wahadhiri wenye kuchukizwa na tabia hiyo ya akina Museveni, waliona ni fursa ya kumtumia Nyerere kuwaumbua USARF hadharani kwa sababu za kupishana mitazamo kiitikadi.
Ukumbi wa Nkrumah ulijaa, Nyerere alipomaliza kutoa hotuba tangulizi, Museveni mwenyewe alishangazwa kusikia ikitamkwa na Makamu Mkuu wa Chuo: " The first questioner is Yoweri Museveni..." ( Sowing The Mustard Seed, pg, 27)
Museveni analikumbuka swali lake, lilihusu Ujamaa. Kwamba Nyerere alikuwa na maana gani katika Ujamaa anaouzungumzia. Museveni alianza kwa kumshambulia Nyerere juu ya dhana ya Ujamaa kwa kadiri anavyoiwasilisha yeye Nyerere.
Kwa Museveni, alisema ina sura ya ujima na haiwezi kukidhi matakwa ya itikadi ya kiuongozi wa kisasa. Kwamba Nyerere anatolea mfano kabila lake ( Wazanaki) kama mfano kwa Watanzania wengine kuwa ni mfano wa jamii ya kijamaa wakati Wazanaki walikuwa chini sana kimaendeleo na hawakuwa na matabaka ya kijamii.
Kwa Museveni, hali halisi haikuwa hivyo sehemu nyingine katika Afrika. Museveni alitoa mifano ya kwao Uganda, ambako hata kabla ya ukoloni kulikuwa na tawala za Kifalme zenye matabaka, kama Buganda. Hivyo, akamwambia Nyerere, kuwa huwezi kusema kuwa Afrika kumekuwa na ujamaa wa watu kuishi kindugu wakati wote. Kwamba ni wakoloni ndio waliokuja kuharibu mfumo huo.
Baada ya Museveni kushusha kigongo hicho, Nyerere alitumia nusu saa kujibu swali la Museveni, lakini, kimsingi, alilizunguka swali la Museveni. Hakulijibu. Mara kadhaa ukumbi ulikuwa ukilipuka kwa vicheko. Nyerere alikuwa mahiri kwenye rhetoric, uwezo wa kuongea hadharani.
Lakini, muda wote, Nyerere hata mara moja hakumponda Museveni wala USARF kama ilivyotarajiwa na Vijana wa TANU na baadhi ya wahadhiri wa Mlimani.
Nyerere akarudi tena Mlimani mara nyingine kuongea na wanafunzi. Siku hiyo vijana wa USARF hawakuingia ukumbini. Nyerere alipomaliza maongezi yake, na wakati akiondoka, alisikika akiwauliza waandaaji:
" Wale jamaa ' USARF' leo sikuwaona!"
Ndio, moyoni, Nyerere aliwaheshimu na aliwapenda USARF. Nyerere alimheshimu na alimpenda Museveni, kwa misimamo yake.
Maggid Mjengwa,
0688 37 36 52 ( Whatsapp)
0754 678 252

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช