Baadhi ya
Vyombo vya habari vya hapa nchini hivi karibuni vilitoa taarifa kuwa,
Watanzania 8 wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa Serikali ya Tanzania
wamekamatwa nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kwenye mgodi wa urani wa
Kayerekera uliopo nchini Malawi kinyume cha sheria.
Taarifa
hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa na chombo cha habari cha Malawi
ambacho kilidai kuwa watu hao wametumwa na Serikali ya Tanzania ili
kuchunguza kama Serikali ya Malawi inatengeneza silaha za nyuklia kwa
kutumia madini ya urani ya kutoka mgodi huo.
Kufuatia
taarifa hizo, Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi
ulifuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Baada ya kufuatilia
ilibainika kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka taasisi ya CARTAS iliyo
chini ya Kanisa Katoliki Songea mkoani Ruvuma walikamatwa na vyombo vya
usalama katika Wilaya ya Karonga ambayo inapakana na Wilaya ya Kyela.
Watanzania
hao mara moja walifunguliwa kesi kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai
la kuingia eneo la mgodi bila kibali (criminal trespass).
Ubalozi
uliwasiliana na Taasisi ya CARTAS kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao
kufanya ziara nchini Malawi. Ubalozi ulielezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa
ni ya mafunzo ambapo walitaka kufahamu juu ya madhara yatokanayo na
machimbo ya madini ya urani. Watanzania hao kwa sasa wapo katika gereza
kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 04 Januari 2017.
Ubalozi
unaendelea kufanya mawasiliano na Kanisa Katoliki Songea ili kupata
maelezo zaidi kuhusu ziara ya watu hao kwa madhumuni ya kuyawasilisha
mamlaka husika ili watuhumiwa waweze kutolewa.Aidha, Wizara kupitia
Ubalozi umebaini kuwa CARTAS iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini
Malawi bila kupata kibali kutoka mamlaka husika na bila kutoa taarifa
Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara hiyo.Aidha, kipindi cha kufanya ziara hiyo
nchini Malawi hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya Malawi
wanakuwa katika likizo ya mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03
Januari 2017. Hii inakwamisha juhudi za kuwafuatilia watu hao ikiwa ni
pamoja na kukwama kwa maombi ya kibali cha kuwatembelea watu hao tarehe
28 Desemba 2016.
Wizara
inatoa wito kwa mara nyingine kwa taasisi za dini, vyuo vya elimu na
watu binafsi kuomba vibali na kufuata sheria za nchi nyingine
wanapofanya ziara za mafunzo au ziara nyinginezo ikiwa ni pamoja na
kuwasiliana na ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya kufahamishwa
taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka
usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wizara,
kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi unaendelea na jitihada za
kuhakikisha kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 29 Desemba 2016.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269