.

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA NA TARATIBU

Dec 2, 2016

Benjamin Sawe-MAELEZO
Rai imetolewa kwa watumishi wa Umma kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria na taratibu ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano ya kuwahudumia wananchi ili kukabiliana na umasikini.
Akizungumza na Maelezo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva amesema miaka michache baada ya uhuru kumekuwa  na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya baadhi ya viongozi wa Umma kuhusu huduma zisizoridhisha,ubadhirifu wa mali za umma,matumizi mabaya ya madaraka ,wizi na ukiukwaji wa haki za binadamu
Amesema kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, kumeleta mabadiliko kwa watendaji wa umma katika ngazi mbalimbali za kimamlaka ukitofautisha na miaka ya nyuma ambapo baadhi ya watendaji walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea.
“Viongozi wengi wa umma walikuwa wakifanya kazi bila kujali wajibu wao na wala hakukuwa na uwajibikaji badala ya kuwatumikia wananchi wakawa wanatumikia matumbo yao.”Alisema Bw. Lyaniva
Alisema Rais Magufuli ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi ya kuwaondoa madarakani viongozi wazembe, wasiowajibika na wasiokuwa na uwezo wa kufanya kazi katika kuwatumia wananchi.
Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inastahili pongezi kwa hatua inazochukua katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi ikiwemo uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi nchini, kwani hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana katika nchi pasipo na kupiga vita rushwa.
“Ni wajibu wa kila mwananchi kuichukia rushwa kwa vitendo ikiwemo kuwafichua hadharani kikundi cha watu kinachojihusisha na rushwa kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo.” Alisema Bw. Lyaniva.
Bw. Bright Kalamba (68) mkazi wa Ubungo Msewe amesema mara baada ya uhuru watumishi wa umma walikuwa na maadili katika utendaji wa kazi hali ambayo ilileta matumaini kwa wananchi walioichagua Serikali iliyopo madarakani.
Alisema licha ya changamoto mbalimbali za baadhi ya watumishi wa umma kutokuwa na maadili katika awamu zilizopita, ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia maadili ya watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.(P.T)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช